Habari Mseto

Hospitali ya Thika yaimarisha mikakati kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19

July 14th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Thika Level 5 inaendelea kujiandaa kuweka vitanda vya wagonjwa wa Covid-19.

Msimamizi mkuu wa hospitali hiyo Dkt Jesse Ngugi alisema tayari wameweka vitanda 13 vya wagonjwa hao huku wakitarajia kuongeza vingine 20 ili kukabiliana na janga hilo.

Alisema hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 700 kufikia 1,000 kwa siku huku wagonjwa wengi wakitoka kaunti jirani.

Alisema wagonjwa wengine hutoka Kitui, na hata Murang’a ili kutafuta huduma.

Hata hivyo, alisema hivi majuzi walipata wagonjwa 30 walioambukizwa Covid 19.

Sita waliwekwa katika wadi.

Wagonjwa 25 walipona, huku mmoja akifariki.

“Hata hivyo tunajaribu kuwashughulikia wagonjwa walioko jinsi tuwezavyo, wauguzi wakifanya kazi ya ziada,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema Kaunti ya Kiambu imefanya juhudi na kuweka vitanda 230 katika hospitali ya Tigoni Level 4 huku hospitali ya Wangige ikiwa na vitanda 150.

Alisema Wizara ya Afya inafanya mikakati kuona ya kwamba wauguzi wanapata mafunzo maalum jinsi ya kukabiliana na wagonjwa wa Covid-19.

“Wakati huu tunapokabiliana na Covid-19 tunahakikisha kila muuguzi anavalia mavazi ya kujikinga – PPE – ili wawe salama.

Alisema kaunti ya Kiambu inafanya mipango ili kuweka vitanda 150 katika hospitali ya Ruiru Level 4.

“Hapa katika hospitali ya Thika Level 5 tumeweka mikakati maalum kuona ya kwamba kila mtu anayeingia katika eneo hilo ananawa mikono, anavalia barakoa, kuweka nafasi ya mita chache kutoka alipo hadi kwa mwenzake na pia tunapima joto la mwili,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema katika hospitali hiyo, kuna mitambo ya kisasa aina ya Digital XRay, Citi Scan, na Utra Sound ambayo inafanya kazi kwa ubora wa hali ya juu.

“Tayari tumeboresha sehemu ya wajawazito kujifungua; yaani mataniti ambako kuna vitanda 200 vya kisasa. Wanawake wanaofika eneo hilo wanahudumiwa vyema na wauguzi waliohitimu,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema hospitali hiyo tayari imefanya ushirikiano wa kikazi na Chuo Kikuu cha Mount Kenya, pamoja na shirika la kufanya utafiti wa kimatibabu nchini la Kemri.