Habari za Kaunti

Hospitali yachunguzwa kwa utepetevu uliosababisha mtoto kukatwa mkono

March 20th, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

BARAZA la Uuguzi Nchini limeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu madai ya utepetevu katika hospitali ya Wesu iliyoko katika eneo la Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, ambapo inadaiwa ilisababisha mkono wa mtoto mchanga kukatwa.

Baraza hilo limeanza kuchunguza kesi hiyo na kwa sasa limeomba rasmi idara ya Afya ya kaunti hiyo kutoa stakabadhi na maelezo yanayohusiana na tukio hilo lililotokea mnamo Januari mwaka huu.

Katika barua iliyotumwa kwa waziri wa Afya katika Kaunti ya Taita Taveta Gifton Mkaya, baraza hilo limeomba nakala zilizothibitishwa za ratiba za zamu za wafanyakazi wote katika wodi ya kujifungua ambapo tukio hilo lilitokea mwezi Januari na Februari, taarifa kutoka kwa muuguzi mkuu wa wodi hiyo, wauguzi waliokuwepo, na daktari au msimamizi wa kituo cha afya.

Baraza hilo pia limesema litafanya ukaguzi wa ripoti za vifo vilivyotokea katika kituo hicho na kupitia stakabadhi zote zinazohusiana ili kubaini matukio yaliyopelekea vifo hivyo.

“Baraza litafanya ukaguzi wa ripoti za vifo vya kituo na kupitia nyaraka zote. Tutawasiliana zaidi baada ya kupitia kesi hizi,” ilisema barua hiyo iliyosainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Anne Mulaki.

Uchunguzi huo unatarajiwa kufichua yaliyojiri hadi kupelekea kukatwa kwa mkono wa kulia wa mtoto huyo wa siku kumi na moja.

Tukio hilo lilitokea baada ya mhudumu mmoja kusahau glovu kwenye mkono wa mtoto, ambayo ilitumika kusaidia kuweka katheta kwa ajili ya kumpa dawa baada ya mtoto huyo kuugua.

Glovu hiyo iligunduliwa baada ya saa 36, ambapo kufikia wakati huo mkono ulikuwa umeanza kuoza.

Ili kuokoa maisha yake, mtoto huyo alihamishiwa hadi hospitali ya Makadara jijini Mombasa ambapo mkono wake ulikatwa.

Kufikia sasa, idara ya afya ya kaunti hiyo ilisema kuwa hatua za kinidhamu zimechukuliwa dhidi ya wahudumu wa afya waliozembea.

Kufuatia tukio hilo, waziri Mkaya alitangaza kuwa idara hiyo imewasimamisha kazi wahudumu wanne waliotuhumiwa kwa utepetevu huo. Waliofutwa kazi ni pamoja na wauguzi watatu na mhudumu wa kliniki aliyeweka katheta hiyo.

Katika mahojiano ya awali, Bw Mkaya alikiri kwamba kulikuwa na uzembe kutoka kwa wahudumu hao wa afya.

“Tuliwasimamisha kazi kwa sababu wagonjwa hawatakuwa na imani na huduma zao,” alisema katika mahojiano na wanahabari.

Waziri huyo alisema baada ya kutambua hali ya mkono wa mtoto, wahudumu walijitahidi kadri ya uwezo wao kuuokoa.

“Kwanza alipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Moi huko Voi kisha hadi hospitali Coast General kwa sababu tulikuwa tunajaribu kuokoa mkono na hatukuwa na wataalamu wa kufanya upasuaji huo,” alisema.

Visa vya utepetevu vimekuwa vikiripotiwa katika baadhi ya vituo vya afya vya kaunti hiyo.

Katika tukio lingine lililotokea mwezi Oktoba 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Moi iliyoko mjini Voi, mtoto wa umri wa miaka minane alifariki baada ya kusubiri kwa takriban saa tisa kupigwa picha ya ‘CT scan’.

Daktari aliyekuwa akimhudumia alipofika katika kituo hicho cha matibabu alikuwa amemtuma mtoto huyo kufanyiwa CT scan ili kubaini chanzo cha maumivu makali kwenye jicho lake la kulia. Hata hivyo, familia ilidai kuwa afisa aliyekuwa anatarajiwa kupiga picha hiyo alichukua mda mrefu kufika.

Familia ya mtoto huyo ililaumu hospitali hiyo kwa uzembe lakini hadi leo, hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa dhidi ya wahudumu husika.

Hata hivyo, hospitali hiyo, kupitia Bw Mkaya, ilikanusha madai hayo ikisema hakukuwa na uzembe kwa upande wao na kudai kuwa mtoto huyo alikuwa akiugua ugonjwa wa leukemia ambao ulisababisha kifo chake.