Habari Mseto

Hospitali yajitetea kuhusu mama kubeba mtoto mfu hadi mochari

February 19th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

IDARA ya Afya katika Kaunti ya Nairobi imekanusha habari kuwa usimamizi wa hospitali ya Mbagathi ulikataa kumhudumia mwanamke ambaye alilazimika kutembea kilomita tano akiwa amebeba mwili wa mwanawe aliyekufa hadi mochari ya City wiki iliyopita.

Kaimu Waziri wa Afya wa Kaunti ya Nairobi, Charles Kerich alieleza jana kuwa Immaculate Auma alitoka hospitalini humo wakati usimamizi wake ulipokuwa ukifanya mpango wa kupata gari la kusafirisha mwili wa mwanawe na wahudumu hawakukataa kumpa usaidizi jinsi ilivyodaiwa.

Bw Kerich alisema wafanyakazi wa hospitali hiyo hawafai kulaumiwa kwa kuwa Bi Auma na mtoto huyo hawakulazwa hospitalini humo wala mwanawe hakufariki akipokea matibabu katika hospitali hiyo.

“Bi Immacualate na mtoto wake hawakulazwa katika hospitali ya Mbagathi, na baada ya uchunguzi tumebaini kwamba wafanyakazi hawakufanya kosa lolote.

“Uchunguzi kuhusu kisa hicho sasa umekamilika na hakuna mfanyakazi aliyepatikana na hatia ya kutelekeza majukumu yake na kutompa msaada,” akasema Bw Kerich kwenye kikao na wanahabari hospitalini humo jana.

Waziri huyo hata hivyo alikiri kwamba kuna haja ya kuboresha huduma katika hospitali hiyo kwa kuziba mianya kadhaa inayolemaza utendakazi wa wahudumu na vitengo mbalimbali vya afya.

“Miili inayoingizwa hapa itahifadhiwa katika chumba cha maiti baada ya walioileta kupiga ripoti kwa polisi. Kutolewa kwa cheti cha mazishi kutafanywa na mochari ya City na iwapo kuna hitaji la kufanywa kwa uchunguzi wa maiti basi wafanyakazi wetu watawajibikia hilo baada ya kupokea mwongozo maalum kutoka kwa usimamizi,” akaongeza Bw Kerich.

Alitaja kusambaratika kwa mfumo bora wa mawasiliano, maafisa wa usalama kukosa kutilia maanani majukumu yao na hospitali kukosa kumiliki gari la kusafirisha miili kama baadhi ya changamoto zinazokabili hospitali hiyo, lakini akasema matatizo hayo yanashugulikiwa na usimamizi wake kwa ushirikiano na serikali ya kaunti.