Habari Mseto

Hospitali zisizotibu wanafunzi kuona cha moto

June 16th, 2019 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WIZARA ya Elimu imezionya hospitali ambazo zinawanyima wanafunzi huduma ya afya kwa kukosa kusajiliwa katika mfumo wa Nemis, ikisema kwamba zitachukuliwa hatua.

Ili wanafunzi wanufaike na bima ya afya (NHIF), ni sharti wasajiliwe kwenye Nemis. Hata hivyo, maelfu ya wanafunzi ambao hawajasajiliwa katika Nemis wamekuwa wakinyimwa huduma za afya wanapougua wakiwa shuleni.

Walimu wakuu walitoa wito kwa serikali kushughulikia changamoto hiyo.

Ukosefu wa cheti cha kuzaliwa ni changamoto ambayo wanafunzi hasa wa maeneo ya mashambani wanakumbana nayo na kuwazuia kusajiliwa katika Nemis. Kulingana na wizara hiyo, kati ya wanafunzi milioni 2.9 nchini, ni 2.6 milioni ambao wamesajiliwa katika mfumo wa Nemis.

Lakini Waziri wa Elimu Prof George Magoha aliagiza huduma za afya kuwatibu wanafunzi wote bila ya ubaguzi.

“Mtoto yeyote ambaye hajasajiliwa katika Nemis, akiugua na ameenda hospitalini, sharti atibiwe, bora tu kuna ushahidi kwamba yeye ni mwanafunzi,” Prof Magoha alisisitiza.

Akiongea kwenye kongamano hilo la walimu wakuu, Prof Magoha alionya kuwa endapo mwanafunzi atanyimwa huduma za afya, hatua zitachukuliwa kwa kituo cha afya” alisema Prof Magoha.

Hii ni afueni kwa wazazi na walimu kwani wanafunzi wote watapokea matibabu wanapougua shuleni.

Akiongea mjini Mombasa wakati wa kufunga mkutano mkuu wa walimu wakuu wa shule za upili za umma nchini, Katibu katika wizara ya Elimu, Dkt Belio Kipsang, alisema wizara yake itatumia Sh59 bilioni kufadhili elimu ya wanafunzi wa shule za sekondari mwaka huu.