Habari MsetoSiasa

Hoteli Kakamega zatarajia mavuno Mashujaa Dei

October 18th, 2018 1 min read

Na BENSON AMADALA

Wamiliki wa hoteli mjini Kakamega wamesema kuwa wamejitayarisha vya kutosha kuvuna kutokana na hafla ya kuadhimisha Sikukuu ya Mashujaa itakayofamyiwa humo Jumamosi.

Sherehe hizo zitahudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto na maafisa wa serikali kuu, serikali za kaunti, wajumbe na wananchi wa kawaida.

Zaidi ya kutoa malazi na chakula, wamiliki wa mahoteli wamebuni ratiba ya burudani kwa wote watakaohudhuria sherehe hizo.

Wamiliki hao wakiongozwa na mwenyekiti Mchungaji William Ouya walisema wametambulisha maeneo ya kitalii na kitamaduni kwa lengo la kuwaburudisha wageni mjini humo.

“Tumebuni burudani kwa wageni wetu ikiwemo ni pamoja na kutembelea maeneo ya kitamaduni na kitalii katika kaunti hii,” alisema Bw Ouya.

Baadhi ya maeneo maarufu ni pamoja na jiwe lililo maarufu kwa kulia (Crying Stone) katika eneo la Ilesi, katika barabara ya Kakamega kuelekea Kisumu, mapigano ya fahali eneo la Malinya, eneo Bunge la Ikolomani na Kituo cha Kitamaduni cha Nabongo eneo la Elureko, ambako kulizikwa mfalme wa Wanga, Nabongo Mumia, katika Eneo Bunge la Matungu.

Ada ya hoteli mjini Kakamega ni Sh1500 kwa chumba kimoja na Sh2, 500 kwa vyumba viwili.

Afisa msimamizi katika Hoteli ya Friends, katika barabara ya Kakamega kuelekea Mumias alisema vyumba vyote hotelini humo tayari vimehifadhiwa.

Mchungaji Ouya alisema walikuwa wakitarajia biashara nzuri wakati wa sherehe hizo zitakazofanyika katika uwanja wa Bukhungu.

Jumapili, msemaji wa Ikulu Kanze Dena wakati wa hotuba kwa wanahabari katika Ikulu ndogo ya Kakamega alisema Rais Kenyatta atazungumzia suala la sekta ya sukari ambayo imedhoofika, suala ambalo viongozi wa eneo hilo wameitaka serikali kusuluhisha ili kuimarisha tena sekta hiyo.