Habari

Hoteli ya DusitD2 yafunguliwa baada ya zaidi ya miezi sita

July 31st, 2019 1 min read

Na BRIAN OKINDA na HILLARY KIMUYU

HOTELI ya DusitD2 iliyoko Riverside Drive, Westlands, Nairobi imefunguliwa Jumatano baada ya kufungwa kwa zaidi ya miezi sita tangu shambulizi la kigaidi la Januari 15, 2019, katika DusitD2 Complex lililosababisha vifo vya watu 21.

Sherehe za ufunguzi zimeshuhudia kupandishwa bendera tatu na mwanariadha nguli David Rudisha na mkuu wa hoteli hiyo yenye matawi mbalimbali.

Hoteli hiyo ambayo inamilikiwa na raia wa Thailand ilisalia imefungwa tangu tukio la shambulizi la kigaidi ambalo kundi la al-Shabaab lilikiri kuhusika.

Imekuwa ikikarabatiwa.

Hoteli hiyo ambayo imekodisha asilimia kubwa ya vyumba vilivyoko 14 Riverside Complex ilisalia imefungwa licha ya afisi za biashara nyinginezo kufunguliwa.

Sasa umma utaanza kupata huduma katika hoteli hiyo kuanzia Alhamisi.