Habari Mseto

Hoteli ya Hemingways yajumuishwa kwenye mpango wa hoteli za hadhi

February 27th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

HOTELI ya Hemingways jijini Nairobi, imejiunga na mpango maalum wa Hoteli za Hadhi ya Juu nchini Amerika, maarufu kama ‘AmEx Fine Hotels and Resorts Program‘.

Hoteli hiyo ndiyo ya pekee nchini Kenya kujiunga na mpango huo.

Mpango unashirikisha zaidi ya hoteli 1,000 kote duniani.

Chini ya mpango huo, wanachama huwa wanapata manufaa mengi, baadhi yakiwa pointi na zawadi maalum.

Mkurugenzi Mkuu wa Shughuli katika hoteli hiyo Bw Ross Evans, alisema kwamba hatua hiyo ni dhihirisho la ubora wa huduma ambazo huwa wanatoa.

“Kukubaliwa kwetu kujiunga na Mpango wa Hoteli za Hadhi ya Juu nchini Amerika ni ishara kwamba huduma zetu ni za kipekee na za hadhi ya juu,” akasema Bw Evans.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa wateja ambao wana kadi maalum za hoteli zilizo kwenye mpango huo, watafaidika pakubwa kwa kupewa huduma za kipekee popote walipo duniani.

Manufaa mengine wanayopata ni muda wa kutosha wa kuingia na kutoka, vyumba vya hadhi ya juu na Sh10,000 za kugharimia vyakula na vinywaji.

“Tunafurahia sana kuwa hoteli ya pekee nchini kukubaliwa kwenye mpango huu. Hilo pia litaimarisha nafasi ya Kenya kama kivutio cha watalii duniani,” akasema.

Ili hoteli husika kukubaliwa kwenye mpango huo, huwa inatuma ombi maalum, ambalo baadaye hukaguliwa kwa kina.

Ukaguzi huwa unaikagua hoteli hiyo ikiwa imetimiza viwango vinavyohitajika, kabla ya kukubaliwa.

Kando na Nairobi, hoteli hiyo ina matawi mengine katika maeneo ya Mara na Watamu.