Michezo

Howe aishusha Bournemouth daraja kisha ang'atuka

August 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BOURNEMOUTH wameagana rasmi na kocha wao Eddie Howe baada ya kushushwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Miaka mitano ya Bournemouth katika EPL ilifikia tamati mnamo Julai 26 licha ya wao kuwapokeza Everton kichapo cha 3-1 uwanjani Goodison Park. Sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Aston Villa dhidi ya West Ham United uwanjani London ilihakikisha kwamba Bournemouth wanashuka ngazi kwa pamoja na Norwich City na Watford.

Howe, 42, aliwaongoza Bournemouth katika jumla ya mechi 450 katika awamu mbili za ukocha chini ya miaka 10 iliyopita.

Katika taarifa yake, Howe ambaye ni mzawa wa Uingereza alisema anaamini kwamba “huu ni wakati mwafaka zaidi kwa klabu yake kupata mabadiliko”.

“Baada ya kuhudumu kambini mwa Bournemouth kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita nikiwa mchezaji kisha kocha, kuagana na kikosi hiki ni kati ya maamuzi magumu zaidi ambayo nimewahi kufanya,” akasema Howe.

“Ingawa mapenzi niliyo nayo kwa kikosi hiki yatasalia, nimehisi kwamba huu ndio wakati mwafaka zaidi kwa klabu kupata mwelekeo mpya.”

“Bournemouth watasalia moyoni mwangu daima ila naamini kuwa hiki ndicho kipindi bora zaidi kwa mabadiliko kushuhudiwa,” akaongeza.

Bournemouth walipanda ngazi kwenye Ligi ya Daraja la Pili (League Two) na kuishia kuwa miongoni mwa vikosi thabiti zaidi katika Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) chini ya Howe aliyewaongoza kupanda ngazi mara tatu chini ya kipindi cha misimu sita pekee.

Hata hivyo, walipoteza jumla ya mechi 22 kutokana na michuano 38 ya EPL msimu huu katika matokeo ambayo yaliwaweka katika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa jedwali.

Licha ya kujinasia huduma za wanasoka ghali kwa minajili ya kampeni za EPL msimu huu wa 2019-20, matokeo ya Bournemouth hayakuridhisha chini ya Howe aliyewahi kuwasakatia zaidi ya mechi 250.

Fowadi Jordon Ibe aliwagharimu Bournemouth kima cha Sh2.1 bilioni kutoka Liverpool mnamo 2016. Hata hivyo, aliwajibishwa katika mechi mbili pekee katika msimu wa 2019-20 huku fowadi Dominic Solanke aliyesajiliwa pia kutoka Liverpool kwa Sh2.7 milioni mnamo 2019 akifunga mabao matatu pekee kutokana na mechi 32.

Msimu huu wa Bournemouth katika EPL ulivurugwa pia na wingi wa visa vya majeraha yaliyoshuhudia beki Charlie Daniels akisalia mkekani kwa kipindi kirefu kuanzaia Agosti 2019 huku mfumaji David Brooks akifanyiwa upasuaji mara mbili.