Habari Mseto

Huduma Namba itatumiwa kutoa leseni za kuendesha magari – NTSA

April 11th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA sasa wataweza kupata leseni za kisasa kuendesha magari kwa urahisi kupitia mpango wa usajili wa watu kidijitali, almaarufu Huduma Namba utakapokamilika mwezi Mei.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Usalama Barabarani (NTSA) Francis Meja Jumatano alisema leseni hizo zitatayarishwa haraka kwa kutumia maelezo ya watu yaliko katika mfumo wa Huduma Namba.

“Watu hawatahitaji kuja katika afisi zetu kama wanavyofanya sasa. Kile watafanya ni kulipa popote walipo kisha tutatumia data yake iliyoko katika mfumo wa Huduma Namba kutayarisha leseni yake,” akasema.

“Hii itawezekana baada ya mchakato wa sasa wa usajili kwa Huduma Namba kukamilika na data iliyoko katika mitambo yetu kuoanishwa na data katika mfumo huo,” Bw Meja akaongeza.

Hata hivyo, alisema mpango huo wa utaoji wa leseni mpya ulioanza Januari mwaka huu bado unaendelea katika afisi za NTSA kote nchini.

Mkurugenzi huyo alisema hayo katika majengo ya bunge alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uwezekezaji (PIC) kwa uchambuzi wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Edward Ouko kuhusu matumizi wa pesa katika NTSA katika miaka ya kifedha ya 2015/2016 na 2016/2017.

Alikuwa akijibu swali la ziada kutoka kwa Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa aliyetaka kujua ikiwa utoaji wa leseni za kisasa za kuendesha magari utajumuisha kwenye mfumo wa Huduma Namba.

Katika ripoti yake Bw Ouko alisema ameridhishwa na matumizi ya fedha katika NTSA katika miaka hiyo ya kifedha kwa hakugundua visa vyovyote vya wizi wa pesa za umma.

Mpango wa utoaji wa leseni za kisasa za kuendesha magari sehemu ya juhudi za NTSA za kupunguza ajali za barabarani.

Sifa kuu ya leseni hiyo ni kwamba unawezesha unakili wa idadi ya visa vya ukiukaji wa sheria za barabarani ambazo dereva amehusika navyo. Ikiwa itabainika kuwa dereva amekiuka sheria za barabara au kuhusika katika ajali mara nyingi, NTSA itaweza kumpokonya leseni hiyo mara moja.

Leseni hiyo inagharimu Sh3,000.