Habari

HUDUMA NAMBA: Serikali yakana madai ya wandani wa Ruto

September 25th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imepuuzilia mbali madai ya wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto kwamba mfumo wa usajili wa watu kidijitali (NIIMS) maarufu kama Huduma Namba unasimamiwa na wageni.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa Katibu Msimamizi (PAS) katika Afisi ya Rais Moffat Kangi amesema kuwa mfumo huo umetengenezwa na serikali ya Kenya na unasimamiwa na Wakenya.

Mnamo Alhamisi, wabunge wandani wa Dkt Ruto walidai kuwa kuna njama ya wizi wa kura zake, katika uchaguzi mkuu ujao, kutumia mfumo wa Huduma Namba.

Wakiongozwa na Seneta wa Nakuru Susan Kihika, wabunge wapatao 15 walioandamana na Dkt Ruto katika ziara eneobunge la Kajiado ya Kati, walidai kuwa mfumo huo unawekwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni kwa lengo la kuvuruga data za wananchi.

“Tunajua Huduma Namba inatumiwa kuendesha wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao ili kutupokonya sisi mahasla ushindi. Hii ndiyo maana huu mpango sasa unasimamiwa na wazungu na maafisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS). Hatutakubali njama kama hiyo,” akasema Bi Kihika.

Naye Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba inapangwa ili itumiwe na viongozi fulani kuendesha njama ya wizi wa kura na vitendo vingine vya uhalifu.

“Pesa nyingi za umma zilitumiwa katika awamu ya kwanza ya Huduma Namba. Sasa wanapanga kutumia pesa zingine katika awamu ya pili ya zoezi hilo huku wakipanga malengo machafu ya kisiasa. Tutapinga ubadhirifu kama unaolenga kuwafaidi wachache,” akasema

Naye Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza alipendekeza kuwa fedha zitakazotumiwa katika awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba zielekezwe katika miradi ya kufufua uchumi ulioathirika na janga la Covid-19.

“Hamuezi iba pesa za corona halafu sasa mnataka tuweke maelezo kuhusu mbuzi na kondoo pamoja na watoto eti tuweke kwa Huduma Namba., Hatuwezi kubali mtuibie kura kutumia Huduma Namba,” akasema Bw Barasa.

Naye Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kwa upande wake akasema: “Hao Wazungu ambao wameletwa eti wasimamie mambo ya Huduma Namba ilhali njama ni kuiba kura hatutawakubali. Sisi na ni ninyi Wamaasai tutachukua rungu tuwarudishe kwao.”

Wabunge hao ni miongoni mwa wengine waliandamana na Dkt Ruto katika sherehe za kuwavukisha vijana kuingia utu uzima, kwa jina Olngesher Lool Ilmerishie. Iliandaliwa na ukoo wa Matapato wa jamii ya Maasai.

Lakini jana Bw Kangi alikana madai hayo akisema usajili wa Huduma Namba unalenga kukusanya data ya Wakenya na wageni wanaoishi nchini ili kuwezesha kupata huduma za serikali kwa urahisi na haraka, na “kuzuia visa kadha vya ulaghai, na hauna malengo mengine”.

“Mfumo wa NIIMS ambao ni wa kwanza wa aina yake katika historia ya Kenya ulibuniwa kwa lengo la kunasa data na maelezo mengine kuhusu Wakenya na wageni wanaoishi. Baada ya kusajiliwa, mtu atapewa Huduma Namba kumwezesha kupata huduma za serikali,” Bw Kangi akasema.

Alisema baada ya usajili wa Huduma Namba ulioendeshwa kati ya Mei 25, 2019, na Juni 20, 2019, nchini na ughaibuni, serikali iko tayari kuzindua mfumo mmoja wa kuwatambulisha watu kielektroniki.

“Mitambo yote ya NIIMS imetengenezwa nchini Kenya na inaendeshwa na Wakenya. Hakuna sehemu yoyote ya utekelezaji wa mfumo huo wa Huduma Namba inayoendeshwa na wageni inavyodaiwa na wanasiasa fulani,” Bw Kangi akaongeza.

Afisa huyo alisema zaidi ya asilimia 90 ya maelezo/data yaliyokusanywa kutoka kwa Wakenya 37 milioni wakati wa awamu ya kwanza ya usajili imesafishwa na kuoanishwa.

“Isitoshe, shughuli ya utengenezaji wa kadi za Huduma itaanza mwishoni mwa mwaka 2020,” Bw Kangi akaeleza.

Kadi za Huduma, akaeleza, zitapigwa chapa (kisha zitolewe) na Wizara ya Masuala ya Ndani katika kituo maalum cha kisasa cha data ‘yenye mitambo ya kuhakikisha usalama wa maelezo kwenye kadi hizo.”

Bw Kangi aliwaonya Wakenya kujihadhari na habari za kupotosha zinazosambazwa kuhusu mpango wa usajili wa Huduma Namba.

Majuma mawili yaliyopita Katiba kati Wizara ya Masuala ya Ndani Karanja Kibicho aliwahikikishia wabunge kwamba mpango wa utoaji kadi za Huduma Namba unaendelea vizuri na utakamilika mwezi Desemba.

Alitangaza kuwa awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba, ili kuwafikia Wakenya walioachwa nje katika awamu ya kwanza, itaanza Februari mwaka ujao wa 2021.