Habari Mseto

HUDUMA NAMBA: Wahudumu wakiri kulemewa na kazi

May 16th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAHUDUMU wanaoendeleza usajili wa wananchi kupata Huduma Namba Ukanda wa Pwani wamekiri kulemewa kuhudummia idadi kubwa ya wakazi wanaoendelea kujitokeza kwa wingi kupita kiasi vituoni ili kusajiliwa katika kipindi hiki cha lala salama.

Afisa Mshirikishi wa Huduma Namba Ukanda wa Pwani, George Lugo, anasema tangu Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kutangaza kwamba hakutakuwa na muda wowote utakaoongezwa kwa usajili wa wananchi kupata Huduma Namba, vituo vingi kote Pwani vimekuwa vikishuhudia milolongo mirefu ya wanaojitokeza kutafuta usajili huo.

Mnamo Jumatatu, Waziri Matiang’i aliweka wazi kwamba shughuli inayoendelea kote nchini ya kusajili watu kwa Huduma Namba itafikia ukingoni Jumamosi Mei 18 na kwamba serikali haitarefusha muda huo.

Bw Matiang’i aidha alitangaza kwamba muda wa mwisho kwa wakenya wanaoishi nje ya nchi kujisajili ni Juni 20 mwaka huu.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali Alhamisi, Bw Lugo alisema tayari Wapwani milioni 2.5 wamesajiliwa kwa Huduma Namba katika kaunti zote sita za eneo hilo, ikiwemo Mombasa, Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Lamu na Tana River.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 63 ya wakazi wote wa Pwani waliosajiliwa kufikia sasa.

Shughuli ya usajili wa Huduma Namba ikiendelea eneo la Mkunguni, Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

 

Bw Lugo alisema idadi hiyo huenda ikagonga milioni 3 kufikia mwishoni mwa shughuli hiyo Jumamosi hii.

Aidha alitaja Kaunti ya Tana River kuwa eneo linaloongoza kwa asilimia kubwa ya wale waliosajiliwa kupata Huduma Namba ikilinganishwa na kaunti zingine za Pwani.

Kaunti ya Tana River iko na zaidi ya wakazi 200,000, ambapo asilimia 70 ya wakazi hao tayari walikuwa wamesajiliwa kwa Huduma Namba kufikia Jumatano wiki hii.

Bw Lugo aidha alieleza wasiwasi wake kwamba huenda wakenya wengi eneo la Pwani wakakosa kujisajili kwa Huduma Namba kufuatia muda mfupi uliobakia wa zoezi hilo kufikia ukingoni.

Alieleza haja ya serikali kusongesha muda ili wananchi wengi zaidi waweze kuandikishwa kwa Huduma Namba.

“Tayari tumeanza kushuhudia misongamano ya watu ambayo hatuwezi kuimudu vituoni. Tangu waziri Matiang’i kutangaza kutokuwepo kwa nyongeza yoyote ya muda kwa shughuli ya Huduma Namba, wananchi wamejitokeza kwa wingi vituoni ili kutafuta usajili.

“Wasiwasi wetu ni kwamba ikiwa serikali haitaongeza muda kama ilivyotangaza, Wapwani wengi wataachwa bila kusajiliwa. Watu wanojitokeza ni wengi lakini kwa upande mwingine muda uliobakia nao ni mfupi mno,” akasema Bw Lugo.

Msimamizi wa Huduma Namba Ukanda wa Pwani, George Lugo, Asema zaidi ya wapwani milioni 2.5 wamesajiliwa kwa Huduma Namba na kwamba nambari huenda ikagonga milioni 3 kufikia mwishoini mwa zoezi hilo Jumamosi. Picha/ Kalume Kazungu

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, aliwapongeza wakazi wa Lamu na viongozi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha shughuli ya usajili wa Huduma Namba.

Bw Kanyiri alisema watu 105,000 tayari walikuwa wamesajiliwa kwa Huduma Namba kote Lamu kufikia Alhamisi.

Alisema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo mwisho wa zoezi hilo mnamo Jumamosi.

“Zoezi limefana hapa Lamu. Watu wamekuwa wakijitokeza kwa wingi. Kufikia sasa tuko na watu 105,000 ambao wamefaulu kusajiliwa kwa Huduma Namba. Idadi itongezeka na kufikia hata asilimia 85 au 90 kufikia mwishoni mwa zoezi hili mnamo Jumamosi.

“Ombi langu ni wakazi wa hapa kuendelea kujitokeza na kusajiliwa kwa Huduma Namba ili kurahisisha utoaji Huduma za serikali kwa wananchi,” akasema Bw Kanyiri.