Habari Mseto

Huduma Namba yachanganya Wakenya zaidi

November 1st, 2020 2 min read

CECIL ODONGO na VALENTINE OBARA

MASWALI yameibuka upya kama serikali itafanikisha mpango wa Huduma Namba, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mpango wa kukusanya alama za vidole za wananchi kwa sekta ya afya.

Rais Kenyatta jana aliongoza shughuli ya Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), kukusanya alama za vidole za wananchi ikielezwa kuwa hatua hiyo itaboresha utoaji huduma.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF, Dkt Peter Kamunyo, alisema usajili wa alama za vidole utafanyika katika vituo 153 vya NHIF vilivyo maeneo tofauti ya nchi.

“Usajili huu utaboresha uwazi na utoaji huduma. Utahitajika kusajili alama za vidole vyote kumi. Ukitaka kuhudumiwa utahitaji tu nambari ya kitambulisho au ya NHIF kisha uthibitishwe kwa alama ya kidole kimoja,” akaeleza.

Lakini watumizi wa mitandao ya kijamii walitilia doa hatua hii, wengi wakisema ni uharibifu mwingine wa fedha na rasilimali kwani serikali ilikuwa ishakusanya alama hizo wakati ilipokuwa ikisajili watu kwa Huduma Namba.

Utekelezaji wa Huduma Namba ulikumbwa na vikwazo kutokana na kesi zilizoupinga mahakamani, kando na ukosefu wa sheria za kutosha kuhusu mpango huo.

Wakati wa sherehe za Mashujaa Dei, Rais alitangaza kuwa kuna hatua zimepigwa kuufanikisha.Jana, alisema Wakenya milioni moja kutoka jamii maskini watanufaika kwa kulipa ada za Hazina ya Bima ya Kitaifa (NHIF) kama njia ya kufanikisha mpango wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC).

Mpango wa majaribio wa UHC ulizinduliwa mnamo 2018 katika Kaunti ya Kisumu na kuhusisha kaunti za Isiolo, Nyeri na Machakos lakini ukakwama kabla kutekelezwa katika kaunti zote 47. UHC ni mojawapo ya miradi mikuu ya Rais Kenyatta ambayo ananuia kufanikisha kabla aondoke mamlakani mwaka wa 2022.

“Mpango ambao tunazindua leo wa UHC lazima ufanikiwe. Nataka NHIF ihakikishe kwamba pesa za wateja zinatumika vizuri na haziporwi. Tutahakikisha atakayefuja pesa za umma atajutia kitendo chake,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa nchi pia aliwataka wabunge wapitishe sheria zitakazofanikisha utekelezaji wa mpango huo badala ya kulumbana kuuhusu utakapofikishwa kwa mjadala bungeni.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Bw Wycliffe Oparanya, alisema magavana wamejitolea kusaidia serikali kuu kutekeleza UHC, lakini itabidi kaunti zipewe rasilimali zote inazohitaji.? Alisema serikali za kaunti zimejitolea kutenga asilimia 30 ya fedha kwa hazina maalum ya afya, na serikali kuu pia inafaa kuweka hazina maalum ya afya.

“Tumekuwa na sera nzuri sana tangu jadi lakini utekelezaji umekuwa tatizo. Hatuwezi kutekeleza UHC kama hakuna mfumo wazi kuhusu ufadhili wake,” akasema.

Mkutano wa jana ulihudhuriwa pia na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, na magavana wengine akiwemo Gavana Hassan Joho wa Mombasa.

Bw Joho alitoa wito kwa serikali kuu iongeze idadi ya hospitali za umma zinazoruhusu utumizi wa NHIF badala ya kulenga hospitali nyingi za kibinafsi.