HabariSiasa

Huduma Namba yapigwa breki

February 28th, 2019 2 min read

Na IBRAHIM ORUKO

KAMATI ya Bunge la Seneti kuhusu Usalama imewataka mawaziri wawili na Mwanasheria Mkuu kufika mbele yake kufafanua kuhusu kutekelezwa kwa Mfumo wa Uhifadhi na Usimamizi wa Taarifa (NIIMS).

Kamati hiyo inataka utekelezaji wa mfumo huo kusitishwa kwanza, hadi pale mawaziri Fred Matiang’i wa Usalama wa ndani na Joe Mucheru wa Habari na Mawasiliano, pamoja na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara watafika mbele yake kufafanua kuhusu masuala tata.

Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo Johnson Sakaja alielekeza hivyo Alhamisi, baada ya mawaziri hao na Bw Kihara kukosa kufika mbele yake kujibu maswali yaliyoibuliwa na wabunge kuhusu utekelezaji wa mfumo huo, uliogharimu Sh6 bilioni za mlipa ushuru.

Tayari zoezi la majaribio ya utekelezaji wake linaendeshwa katika kaunti 15.

“Tunatarajia mawaziri hao kuchukulia suala hili kwa uzito unaofaa,” Bw Sakaja akaeleza Waziri Msaidizi wa Dkt Matiangi, Patrick Ole Ntutu.

Kamati hiyo ilikuwa imealika maafisa hao katika kikao cha pamoja ambacho kilijumuisha kamati tatu za bunge, ili kujadili suala hilo ambalo limeifanya serikali kuanza kuchukua habari za kibinafsi za watu, japo maseneta wanasema mradi huo hauna msingi kisheria.

Badala ya mawaziri hao kufika, ni Bw Ntutu aliyefika, hali hiyo ikiwaghadhabisha maseneta ambao walidai maafisa hao walikuwa na matharau.

Mradi huo wa serikali unalenga kuwasajili Wakenya wote kidijitali na kuwapa nambari za kipekee zitakazoitwa ‘Huduma Namba’.

Maseneta wanaitaka serikali kuwaeleza Wakenya ikiwa ‘Huduma Namba’ inalenga kuchukua nafasi ya kitambulisho cha kitaifa cha sasa, mbali na kueleza Wakenya namna wataboreshewa huduma kama inavyoahidi.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula alikosoa misingi ya kisheria iliyotumiwa kuja na mfumo wa NIIMS, akisema ni bunge la taifa lililopitisha, bila kuhusisha bunge la seneti.

“Udhibiti wa habari za kibinafsi ni jambo la umuhimu. Mswada wa aina hii ambao una athari hauwezi kupitishwa bila mchango wa bunge la seneti. Sharti utekelezaji wa mfumo wa NIIMS usitishwe kwanza,” akasema Bw Wetangula.

Seneta huyo alisema NIIMS inakiuka haki za watu za usiri, japo kupitishwa kwa sheria hiyo kulipitishiwa bunge la taifa, bila seneti kuhusishwa.

Bw Wetangula sasa analitaka bunge la seneti kutafuta mbinu ya kupendekeza kuwa utekelezaji wa mfumo huo usitishwe kwanza, hadi umma uhusishwe, ukaguzi na upitishiwe bunge la seneti kufanywa sheria.

Seneta wa Baringo Gideon Moi aidha aliunga mkono kuwa sheria hiyo inaingilia haki ya watu kuwa na usiri. Bw Moi alisisitiza kuwa sheria kuhusu udhibiti wa habari za watu za siri inafaa kupitishwa kwanza, kabla ya mfumo wa NIIMS kuanza kufanya kazi.

“Bila sheria ya kudhibiti habari za watu, Wakenya wako kwenye hatari. Utekelezaji wa NIIMS usitishwe hadi sheria kuhusu udhibiti wa habari itakapopitishwa,” Bw Moi akasema.

Suala hilo liliwasilishwa bungeni na seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot wiki iliyopita, akitaka serikali kutoa habari kuhusu sababu za kuingiza mfumo huo, huku akionya kuwa haki za Wakenya zinaweza kukiukwa.

“Tunapoenda katika mikutano ya umma, tunatakiwa na wananchi kueleza kuhusu hiki kitu ambacho kinaingizwa. Ni vyema kwa bunge kupewa habari kuhusu ni kwanini zoezi hili lina umuhimu, manufaa yake kwa taifa na ikiwa haingewezekana kwa habari zilizokuwepo kutumiwa, kinyume na jinsi inafanyika kwa sasa,” Bw Cheruiyot akasema.