Habari Mseto

Huduma za M-Pesa kuzimwa kwa saa 12

July 17th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine wateja wa huduma za kupokea na kutuma pesa kwa njia ya simu; M-Pesa, watakosa huduma hiyo kwa saa 12 kuanzia Jumamosi, Julai 18, 2020 hadi Jumapili, Julai 19, 2020.

Kampuni ya huduma za mawasiliano ya Safaricom imetoa tangazo hilo Ijumaa kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter.

Kampuni hiyo inasema kukatizwa kwa huduma hiyo kutafanyika ili kuipa muda wa “kuimarisha na kukarabati mitambo yetu.”

“Katika muda huo wote huduma zote kupitia M-Pesa kama vile kununua mjazo, kutuma na kupokea pesa hazitakuwepo kwa muda,” kampuni hiyo ikaeleza katika taarifa hiyo.

Ikaongeza: “Marekebisho hayo ya mitambo yamepangwa kufanyika wakati ambapo watu wachache huhitaji huduma hizo. Kwa hivyo, tunatumai sio wengi wataathirika. Hata hivyo, tunaomba radhi kwa usumbufu utakaosababishwa na hali hii.”