Habari Mseto

Huduma za usafiri zakwama mjini Thika baada ya ajali

September 9th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WASAFIRI wa kutoka Thika kuelekea Nairobi mnamo Jumanne jioni walikwama baada ya wahudumu wa bodaboda kufunga barabara kuu ya Thika Superhighway.

Wakati huo pia wahudumu hao walifunga vituo vya magari vya Makongeni, Gatitu, na Witeithie mjini Thika.

Basi la Kenya Mpya lilisababisha ajali ambapo mhudumu wa bodaboda aligongwa na kufariki papo hapo.

Marehemu ambaye ni mwanachama wa 2TKY Sacco, alikuwa kwenye barabara ya Kwame Nkuruma mjini Thika. Waliokuwepo walisema alikuwa akijiandaa kuenda mtaa wa Ngoingwa kumbeba mteja wake.

Hata hivyo basi la Kenya Mpya lilikuwa likiendeshwa kwa kasi na kumgonga na kumtupa mita 30 kutoka barabarani.

Dereva wa basi hilo alipoona hatari kwa kuandamwa na umati wenye hasira, alitoroka kuokoa maisha yake.

Lakini baadaye alijisalimisha katika kituo cha polisi ambako aliandikisha taarifa.

“Hawa madereva wa mabasi huwa hawana nidhamu kwa sababu hiyo sio mara ya kwanza ajali ya aina hiyo kutokea. Huwa wanaendesha magari hayo kiholela,” alisema mmoja wa wahudumu wa bodaboda mjini Thika.

Waendeshaji magari wengi walitafuta barabara za mkato ili kutoka ama kuingia mjini Thika.

Ilibidi maafisa wa polisi kitengo cha trafiki kuingilia kati ili kutuliza mambo katika mji huo.

Maafisa wa polisi walifanya mkutano wa faragha na wahudumu wa bodaboda ambapo walikubaliana ya kwamba dereva huyo wa basi hilo atawasilishwa mahakamani leo Jumatano ili kujibu mashtaka ya kusababisha ajali.

Hata hivyo basi hilo lililosababsha ajali lilipelekwa kituo cha polisi cha Thika huku mwili wa mhanga ukipelekwa hospitali kuu ya Thika Level 5 ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.