Habari Mseto

Huenda ada ya kutoa Sh500 M-Pesa ikaongezeka kutoka Sh28 hadi Sh46

September 19th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

Wakenya wanakumbana na hali ngumu ya maisha, kufuatia mapendekezo kwenye sheria ya kutoza ushuru, ambayo yatapandisha gharama ya kutuma pesa kwa njia ya simu, pamoja kupiga simu na kununua vifushi vya data. 

Mapendekezo hayo ya Rais Uhuru Kenyatta na ambayo yaliwasilishwa mbele ya kamati ya bunge kuhusu bajeti Jumatano yanataka ushuru wa kutuma pesa kwa njia ya simu upandishwe kutoka asilimia 12 hadi asilimia 20, huku ule wa kupiga simu ama kutumia bundles hadi asilimia 15.

Hii ni kumaanisha kuwa anapotoa pesa kutoka M-Pesa Mkenya atalazimika kulipia hadi Sh46 kwa kiwango ambacho sasa kinalipiwa Sh28, huku anayetoa kati ya Sh2,501 na Sh3,500 akilipia hadi Sh83, ilhali kwa sasa ni Sh50.

Ushuru sawia utatozwa wale wanaotumia benki (ATM) kutoa pesa ama kutuma pesa katika akaunti zingine.

Hii ni licha  ya ushuru huo kupandishwa kutoka asilimia 10 hadi 12 miezi miwili iliyopita na waziri wa fedha Henry Rotich.

“Pesa za kutumwa kwa njia za simu, benki na mashirika mengine ya kutuma pesa ama ya kutoa huduma za pesa zitatozwa ushuru wa asilimia 20,” akasema Rais Kenyatta.

Aidha gharama za kutuma pesa zitapanda kutegemea kiwango anachotuma mtu.

Ushuru wa kupiga simu na kutmia mitandao nao utamaanisha kuwa katika kila kadi ya simu ya Sh100, Mkenya atakatwa Sh15 akizitumia kupiga simu ama kununua vifushi vya data.