Michezo

Huenda Bale akarejea Spurs

September 17th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wameanzisha mazungumzo na Real Madrid kuhusu uwezekano wa kumsajili upya fowadi wao wa zamani Gareth Bale ambaye ni raia wa Wales.

Chini ya kocha Jose Mourinho, Tottenham tayari wako pua na mdomo kujinasia huduma za fowadi Sergio Reguilon ambaye amekuwa akicheza na Bale kambini mwa Real.

Bale, 31, aliagana na Tottenham mnamo 2013 kwa kima cha Sh11 bilioni. Tangu wakati huo, amefungia miamba hao wa soka ya Uhispania zaidi ya mabao 100 na kuwashindia mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Bale bado anapenda Tottenham. Ndiko anakotamani kuwa,” akasema Jonathan Barnett ambaye ni wakala wa mwanasoka huyo anayewaniwa pia na Manchester United, Newcastle United na Inter Miami.

Reguilon, 23, ni mwanasoka mzawa wa Uhispania aliyepokezwa malezi ya soka katika akademia ya chipukizi wa Real kabla ya kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza mnamo Oktoba 2018.

Man-United wamekata tamaa ya kumsajili Bale baada ya Real kutaka walipie ada nzima ya kumtwaa nyota huyo. Suitafahamu ya sasa kati ya kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer na Real, imewapa Tottenham fursa ya kuanza kumvia Bale ambaye dalili zote zinaashiria kwamba atarejea London Kaskazini.

Japo Real wana fursa ya kumtoa Bale kwa mkopo, kikosi hicho kinalenga kutafuta fedha zitakazomwezesha kocha Zinedine Zidane kuisuka upya timu yake kwa minajili ya kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kutamba katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mshahara wa Bale huenda kikawa kitu cha pekee chenye uwezo wa kukwaza uhamisho wa sogora huyo kutoka Real kwenda Tottenham. Hadi kufikia sasa, Bale hupokezwa mshahara wa Sh84 milioni kwa wiki.

Kingine ambacho Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy anahofia ni kuvurugika kwa mahusiano miongoni mwa wachezaji na hatimaye kuyumbishwa kwa uthabiti wa kikosi hicho cha Mourinho iwapo Bale atakuwa akipokezwa mshahara mnono zaidi kuliko wa nahodha wa sasa, Harry Kane. Tottenham walimsajili Bale kutoka Southampton akiwa na umri wa miaka 17 pekee.

Katika misimu yake ya kwanza kambini mwa Real, Bale aliridhisha sana akifunga mabao katika fainali mbili za UEFA mnamo 2014 na 2018 na fainali ya Copa del Rey mnamo 2014.

Nyota yake ilianza kudidimia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita baada ya kuanza kuwa mwepesi wa kupata majeraha na uhusiano kati yake na Zidane kuharibika.

Aliwajibishwa na Zidane mara moja pekee baada ya kurejelewa kwa soka ya Uhispania mnamo Juni 2020. Licha ya kuchezeshwa kwa sakika 100 pekee katika msimu mzima wa 2019-20, Real walitwaa ubingwa wa taji la La Liga kwa mara ya kwanza tangu 2017.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO