Michezo

Huenda Gor ikapoteza mastaa sita

June 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

GOR Mahia wanakodolewa jicho na pigo la kupoteza huduma za wanasoka sita wa haiba kubwa ambao mikataba yao inatarajiwa kutamatika mwishoni mwa Juni 2020.

Huku janga la corona na ukosefu wa wadhamini ukizidi kutikisa uthabiti wa kikosi hicho ambacho kimelemewa kabisa kifedha, huenda ikawawia vigumu Gor Mahia kushawishi wachezaji hao kusalia kambini mwao kwa kipindi kingine.

Kati ya masogora matata ambao wako pua na mdomo kuagana na Gor Mahia ni nahodha msaidizi Joash Onyango aliyejiunga nao mnamo 2017, beki Charles Momanyi na mshambuliaji Nicholas Kipkirui.

Wengine ni kapteni Kenneth Muguna, kipa mzawa wa Tanzania, David Mapigano na beki Dickson Ambundo.

Siku chache zimepita tangu mwenyekiti Ambrose Rachier kukiri kwamba wachezaji wa Gor Mahia hawajalipwa mishahara kwa miezi mitano, tukio ambalo lilimfanya kudokeza uwezekano wa baadhi ya masogora wao kuwa wepesi wa kutafufa hifadhi kwingineko.

Hata hivyo, Lordvick Omondi Aduda ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia ni mwingi wa matumaini kwamba usimamizi utaitikia wito wa kocha Steven Polack ambaye ametaka kikosi kufanya lolote liwezekanalo kuwazuia wanasoka hao kubanduka.

Muguna na Onyango wamekuwa wakimezewa mate na miamba wa soka ya Tanzania, Simba SC ambao pia waliwahi kunyakua mvamizi Meddie Kagere na kiungo Francis Kahata kutoka Gor Mahia. Ambundo anahemewa pakubwa na Yanga SC ambao ni watani wa tangu jadi wa Simba katika Ligi Kuu ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mapigano ameapa kutorudi Kenya kuvalia tena jezi za Gor Mahia iwapo mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hawatamlipa malimbikizi yote ya mshahara na marupurupu.