HabariSiasa

Huenda Jumwa na Dori wakapoteza ubunge kwa kuunga mkono Ruto

January 25th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha ODM Alhamisi kiliwatimua wabunge Aisha Jumwa (Malindi) na Suleiman Dori (Mswambweni) kwa kuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Hatua hii inamaanisha kuwa wawili hao wamo kwenye hatari ya kupoteza viti vyao vya ubunge na hivyo kutoa mwanya wa chaguzi ndogo kuandaliwa maeneo yao.

Kulingana na Katiba, mbunge anayevuliwa uanachama kwa njia halali na chama ambacho kilimdhamini kuingia bunge, anapasa kupoteza kiti chake. Hii inaweza kutokana na kuunga mkono chama kingine kwa msingi kuwa mhusika ameacha kuzingatia sera za chama chake.

Lakini kwa sasa Bi Jumwa na Bw Dori wanaweza kupinga hatua ya ODM kwa kuwasilisha rufaa kwa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama ama hata kwenda mahakamani kupinga adhabu dhidi yao.

Hatua ya ODM dhidi ya wabunge hao inatokana na hatua yao mwaka 2018 kutangaza kuunga mkono Dkt Ruto, ambaye ni wa chama cha Jubilee.

Kikao cha NEC hapo jana kiliongozwa na Naibu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya kwa niaba ya kinara Raila Odinga, ambaye alikuwa amesafiri Congo DR kuhudhuria kuapishwa kwa rais mpya Felix Tshisekedi.

NEC ilipitisha wawili hao pia waondolewe katika kamati za bunge. Bi Jumwa ni mjumbe wa Kamati ya Huduma za Bunge (PSC) iliyo na mamlaka ya kuajiri wafanyakazi wa bunge na kuidhinisha masuala yanayohusu maslahi ya wabunge kama vile marupurupu na ziara za ng’ambo.

Mjumbe wa PSC hupokea marupurupu ya vikao ya Sh80,000, afisi, wafanyakazi wa afisini na gari la serikali.

Bw Dori ni mjumbe wa kamati za Leba na Michezo na Kamati ya Masuala ya Mashauri ya Kigeni.

“Baraza la NEC limepitisha mapendekezo ya Kamati ya Nidhamu ya ODM kutaka Bi Jumwa na Bw Dori watimuliwe kutoka chama. Uamuzi huo wa NEC sasa utapelekwa katika Kongamano Kuu la Viongozi wa Chama (NGC) ili uidhinishwe,” akasema Katibu wa ODM, Edwin Sifuna.

Kamati ya Nidhamu ya ODM iliwasilisha ripoti yake mnamo Desemba 4 mwaka jana, ambapo ilipendekeza wabunge hao wawili na madiwani sita watimuliwe.

Uamuzi huo wa NEC unamaanisha kuwa Kiranja wa Wachache Bungeni, Junet Mohamed sasa atamwandikia barua spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi akitaka wawili hao waondolewe kutoka katika kamati za bunge litakaporejelea shughuli zake Februari 12.

Bw Odinga amekuwa akitishia kuwaadhibu wanasiasa wa chama hicho wanaoendesha kampeni za 2022.

NEC hata hivyo ilimwondolea lawama diwani wa bunge la Kaunti ya Busia, Bi Immaculate Joice Adhiambo baada ya kubaini kuwa madai yaliyotolewa dhidi yake hayakuwa na msingi.

Madiwani watano kutoka bunge la Kaunti ya Homa Bay walienda katika Mahakama Kuu ya Kisumu kuzuia chama cha ODM kuendelea kujadili madai dhidi yao hadi pale kesi itakapoamuliwa.