Habari

Huenda Kenya ikose Jaji Mkuu kwa miezi 6

November 26th, 2020 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

KENYA huenda itakaa bila Jaji Mkuu halisi hadi Juni 2021 baada ya jaribio la Tume ya Huduma za Majaji (JSC) kumshinikiza Jaji David Maraga kutoa idhini ya uteuzi wa mapema wa mrithi wake kugonga mwamba.

Jaji Maraga, anayetazamiwa kutoa hotuba yake ya mwisho hii leo (Ijumaa) kuhusu Hali ya Idara ya Mahakama mwakani, anatarajiwa kuanza likizo yake ndefu ya mwezi mmoja mnamo Desemba 14, kabla ya kustaafu kwake rasmi Januari 12, 2021.

Duru kutoka Tume hiyo zilizokataa kutajwa ziliashiria kuwa alikataa pendekezo la makamishna wanane lililomtaka kutia sahihi fomu ya kutangaza kuwepo kwa nafasi, ili Tume hiyo ianze mchakato wa kuteua mrithi wake.

Jaji Maraga imeelezwa alikataa ombi hilo kwa misingi kwamba haliambatani na kanuni na sheria kuhusu kustaafu kwa majaji.

Mchakato wa kustaafu kwa jaji huanza na barua kutoka kwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama inayomwagiza jaji anayeelekea kustaafu kwenda likizo ndefu kabla ya kustaafu.

Msajili Mkuu Anne Amadi alithibitisha Alhamisi kwa Taifa Leo kwamba Bw Maraga alipatiwa barua ya kwenda likizo ndefu mnamo Februari 2020.

“Barua hii (ya likizo ndefu) ilitolewa Februari. Huwa inatolewa mara moja tu,” alisema Bi Amadi.

Mwanzoni mwa mwaka, kulikuwa na ripoti kuhusu Bw Maraga kustaafu mapema kama mtangulizi wake Bw Willy Mutunga, ili kuzuia hali ambapo afisi hiyo kuu zaidi katika Idara ya Mahakama inasalia bila mtu.

Kutokana na muda unaohitajika kisheria kuhusiana na mchakato wa uteuzi wa jaji, huenda Kenya ikasalia bila Jaji Mkuu hadi Juni, 2021.

Endapo hakutakuwa na changamoto zozote na kuchukulia kuwa uteuzi wa mrithi wa Bw Maraga utafanyika pasipo vizingiti vyovyote, tarehe ya mapema zaidi ambayo JSC inaweza kukamilisha uteuzi wa Jaji Mkuu mpya ni Juni 2021.

Sheria haijasema lolote kuhusu iwapo mchakato wa uteuzi wa Jaji Mkuu unaweza kuanzishwa kabla ya wadhifa huo kusaliwa wazi.

Huenda hii ndiyo sababu kundi hilo la makamishna lilimtaka Bw Maraga kutia sahihi fomu ya kutangaza kuwepo kwa nafasi kutoka Tume hiyo ili kuanzisha mchakato huo.

Hii ni kwa sababu anayeshikilia afisi hana mamlaka baada ya kuondoka afisini.

Jaji Mkuu pia anashikilia wadhifa wa mwenyekiti wa JSC.

Kulingana na Sheria kuhusu JSC, mchakato wa uteuzi huanza baada ya Tume kubuni jopo linalojumuisha wanachama wasiopungua watano.