Habari Mseto

Huenda kifungo cha maafisa waliomeza hela za makaburi kikaongezeka

May 22nd, 2018 2 min read

Kutoka kushoto: Aliyekuwa katibu mkuu katika wizara ya Serikali za wilaya Bw Sammy Kirui , aliyekuwa msimamizi wa masuala ya sheria katika baraza la jiji la Nairobi (NCC) Bi Mary Ng’ethe na afisa msimamizi wa idara ya zabuni Bw Alexander Musanga Musee wakiwa mahakamani Mei 21, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

HUENDA waliokuwa maafisa wakuu serikalini waliofungwa miaka mitatu kila mmoja kwa ulaghai wa Sh283 milioni katika kashfa ya kununua shamba la kuwazika wafu Athi River, kaunti ya  Machakos, wakaongezewa kifungo zaidi baada ya kushtakiwa tena pamoja na watu wengine 10.

Aliyekuwa katibu mkuu katika wizara ya Serikali za wilaya Bw Sammy Kirui , aliyekuwa msimamizi wa masuala ya sheria katika baraza la jiji la Nairobi (NCC) Bi Mary Ng’ethe na afisa msimamizi wa idara ya zabuni Bw Alexander Musanga Musee walitolewa gerezani kujibu mashtaka mengine ya hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi aliyeorodhesha kesi hiyo ianze kusikizwa Septemba 10, 2018 hadi Novemba 27, 2018.

Bw Kirui , Bi Ng’ethe na Bw Musee walifungwa pamoja na aliyekuwa katibu wa NCC Bw John Gakuo kwa kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya waliporuhusu malipo ya ununuzi wa ardhi hiyo katika eneo lisilofaa kuzikwa wafu. Wafungwa hao wamekata tufaa.

Watatu hao sasa wameshtakiwa pamoja na mawakili Alphonse Mutinda, Paul Onduso ,  Joseph Owino Kojwado na Newton Osiemo.

Wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Mabw Maina Chege, Nelson Otido, Daniel Mulwa Nguku na Herman Stevens Gavera na kampuni ya Naen Rich Limited.

Washtakiwa hawa walikanusha shtaka la kufanya njama za kuibia Serikali Sh283 milioni katika kashfa ya ununuzi wa shamba la kuwazika wafu katika kaunti ndogo ya Athi River kati ya Desemba 2008 na Aprili 2009.

Wakili Wilfred Nderitu azungumza na mateja wake Mary Ng’ethe mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Na wakati huo huo mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji alikataa pendekezo la wakili Bw Mutinda la kusuluisha kesi hiyo nje ya mahakama.

Bw Mutinda ndiye alikuwa wakili wa mwenye shamba hilo lililokataliwa na serikali kwa kuwa limejaa mawe.

“Ombi la Bw Mutinda kusuluhisha kesi hii nje ya mahakama  imekataliwa na DPP. Nimeamriwa nianze kuita mashahidi katika kesi hii,” Kiongozi wa mashtaka Bw Nicholas Mutuku alimweleza hakimu.

Bw Mutuku alieleza mahakama kwamba ameorodhesha mashahidi 32 watakaochukua muda wa siku sisizopungua 75.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao walimweleza hakimu kuwa watahitaji jumla ya masaa 301 kuwahoji mashahidi watakaofika kortini.

Pia hakimu aliwamuru mawakili wafungue mtandao wawe wakiwasiliana na mahakama jinsi kesi itakavyokuwa inaendelea.

Bw Mugambi alimwagiza Bw Mutuku awakabidhi mawakili 12 wanaowatetea washtakiwa hao nakala za mashahidi waandae utetezi wa washtakiwa hao mapema.

Bw Muagmbi pia aliwataka mawakili wajiepushe na kuomba kesi hii iahirishwe ndipo isikizwe na kuamuliwa ikitiliwa maanani imekaa miaka minane kabla ya kuanza kusikizwa.