Habari MsetoSiasa

Huenda mkutano wa Raila na Moi ukageuza kibao cha mbio za Ikulu 2022 – Wadadisi

April 12th, 2018 2 min read

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga akaribishwa nyumbani kwa rais mstaafu Daniel Moi na mwanawe na pia senata wa Baringo Gideon Moi. Picha/ Hisani

Na PETER MBURU

KINARA wa upinzani Bw Raila Odinga Alhamisi alimtembelea Rais wa zamani Mzee Daniel Toroitich Arap Moi nyumbani kwake eneo la Kabarak, katika ziara isiyotarajiwa.

Ziara hiyo ilijiri siku mbili baada ya Bw Odinga kufanya kikao na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo katika ofisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi.

Kulingana na habari zilizotolewa katika ukurasa rasmi wa facebook wa Bw Odinga, viongozi hao wawili walizungumzia masuala muhimu kuhusu ‘hali ya taifa la Kenya na utulivu’.

Aidha, mwanawe rais huyo wa zamani na aliye pia seneta wa Baringo Gideon Moi, seneta wa Vihiga George Khaniri, mbunge wa Mvita AbdulSwamad Sharrif na Katibu Mkuu wa KANU Nick Salat ni baadhi ya viongozi walioungana na Bw Odinga na Mzee Moi.

“Asubuhi ya leo Mheshimiwa Bw Odinga alimtembelea rais wa zamani Daniel Toroitich Arap Moi nyumbani kwake Kabarak.

Viongozi hao walizungumzia hali ya taifa la Kenya na utulivu. Rais Moi alirejea nchini kutoka ziara ya matibabu hivi majuzi na Bw Odinga akamtakia afueni. Seneta wa Baringo Gideon Moi na Nick Salat walikaribisha wageni.

Viongozi wengine walikuwa Bw George Khaniri na Bw Abduslwamad Sharrif Nassir,” ikasoma habari katika ukurasa wa Facebook wa Bw Odinga.

Viongozi hao aidha walipiga picha nyingi na kuzichapisha kwenye ukurasa wa Bw Odinga, kisha baadaye zikasambaa mitandaoni.

Na japo hawakuzungumza na waandishi wa habari, viongozi hao walifanya kikao cha saa kadhaa ambacho mazungumzo yake hayakubainika.

 

2022

Ziara hiyo hata hivyo imechukuliwa na wadadisi wa masuala ya siasa kama mrengo unaojiunda na kuhusishwa na siasa za uongozi wa nchi na uchaguzi wa 2022, haswa ikijia siku mbili baada ya Bw Odinga kukutana na Bw Kabogo kwa kikao sawia.

Kulingana na wakili Bernard Kipkoech Ngetich, mkutano baina ya viongozi hao wawili haukutarajiwa, namna tu uwiano baina ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta uliwapata wengi bila matarajio, huku akiwataka wakenya kutarajia mabadiliko mengi ya aina hiyo kisiasa kutokea siku zijazo.

“Bado wakenya wana mengi ya kuona, siasa za nchi hii zimejaa hatua za mishtuko kuhusiana na uchaguzi wa 2022 na hatua kadhaa zisizotarajiwa zitachukuliwa hapa mbele. Hakuna aliyetarajia Raila kupatana na Rais Kenyatta wala Mzee Moi lakini hayo yamefanyika,” wakili huyo akasema.

Aliwataka wakenya kujitayarisha kwa mrengo wa aina yake kwa siasa za urais 2022, kwani kulingana naye uwanja wa siasa unabadilika kwa kasi na kwa njia zisizotarajiwa.