Habari

Huenda NHIF ikaanza kufadhili huduma zote

April 11th, 2018 2 min read

Na LUCY KILALO

SERIKALI inafanyia majaribio mpango wa kuhakikisha bima ya kitaifa ya matibabu (NHIF) inashughulikia huduma zote za matibabu.

Waziri wa Afya Sicily Kariuki alisema tayari, mpango huo unafanyiwa majaribio katika Kaunti nne – Nyeri, Machakos, Kisumu na Isiolo.

“Madhumuni ni kuhakikisha kwamba, tunaziba mapengo na kufanya utafiti kuonyesha sehemu zinazohitaji kuboreshwa kwa NHIF,” aliongeza.

Alisema katika muda wa wiki tatu zijazo, serikali italezea ikiwa muda wa kusubiri kusajiliwa kwa NHIF utapunguzwa na kuwezesha Wakenya kupata bima hiyo mara moja.

Wanaojisajili kwa bima hiyo huhitajika kusubiri kwa siku 60 kabla ya kuanza kuitumia. Bi Kariuki alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wabunge.

Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Tharaka Nithi, Beatrice Nkatha alikuwa amesema muda huo wa kusubiri siku 60 ni mrefu mno na baadhi wanahitaji kupata huduma hiyo.

“Inawezekana kupunguza muda kutoka siku 60 hadi 30. Lakini suala hilo nimelielekeza kwa bodi ya NHIF kuangalia uwezekano wake,” waziri aliambia kamati, huku afisa mkuu wa NHIF, Bw Geoffrey Mwangi akisema jibu kamili litapatikana katika muda wa majuma matatu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi Sabina Chege, alitaka kujua ikiwa bima hiyo inaweza kuimarishwa na kuwa ndiyo pekee inayotoa huduma hiyo nchini.

Hata hivyo, waziri alieleza kuwa wameangalia nchi nyingine kama Thailand na Afrika Kusini, lakini wanalenga kujifunza na kuona jinsi ya kuboresha bima hiyo kulingana na hali ya humu nchini na sio kuiga nyingine moja kwa moja.

 

Usisafiri mbali

Pia akijibu swali la mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki, Bw David Gikaria kutaka kuwepo kwa vituo kadha vya usajili wa NHIF kwa wazee wa zaidi ya miaka 60, Bi Kariuki alisema hakuna Mkenya anastahili kusafiri mbali kusajiliwa.

“NHIF ina matawi 62 nchini, matawi 37 madogo pamoja na kupatikana kwa kila kituo cha Huduma. Vile vile, tupo kwa hospitali kadha na hakuna Mkenya anastahili kusafiri mbali kutafuta huduma hiyo,” alisema.

Baadhi ya wanakamati walitaka kujua jinsi Wakenya wanaweza kuhamasishwa zaidi kuhusu bima hiyo, hatua ambayo huenda ikapunguza hafla za uchangishaji pesa wanazolazimika kuhudhuria kila wakati.

Wakati huo huo, mbunge wa Tongaren, Dkt David Eseli aliitahadharisha NHIF kutofuata maagizo ya kisiasa bila kuthibitisha ufaafu wake.

“Mkiamua kufuata maagizo ya kisiasa huenda mkafeli. Lazima muwe na ushahidi kamili kuhusu matokeo yake,” alisema.

Naibu Rais William Ruto alitangaza majuzi kuwa Sh4 bilioni zimetengwa kutoa bima hiyo kwa wanafunzi milioni tatu wa sekondari.

Serikali inatarajiwa kutenga Sh1,999 kwa kila mwanafunzi. Hata hivyo, baadhi ya maswali ibuka ni kuwa wanafunzi hao hudhaminiwa na wazazi wao wanapojisajili kwa bima hiyo.