Michezo

Huenda pasitokee rais atakayempiku Moi katika kufadhili michezo

February 9th, 2020 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Haipingiki kuwa rais wa pili wa Kenya, Daniel arap Moi atakayezikwa Jumatano nyumbani kwake Kabarak, Nakuru ameacha jina kubwa kwenye sekta ya michezo.

Juhudi, ari na mapenzi yake kwa spoti yamedhihirisha kwamba ni miongoni mwa viongozi wachache duniani waliojizatiti kuimarisha miundomsingi mbalimbali ya michezo hasa viwanja.

Miundomsingi kama uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani pamoja na Nyayo ni ithibati kuwa itakuwa vigumu kumpata rais atakayemfikia katika wanda la spoti.

Hakuna maneno ya kutosha kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia ya spoti. Kifo chake kimewaguza wengi hasa wale walionufaika kutokana na mchango wake alipokuwa usukani kwa muda wa miaka 24.

Kati ya marais waliotawala Kenya baada ya taifa hili kupata uhuru, mchango wa marehemu Moi kuhusiana na michezo hauna kifani.

Mzee huyo aliongoza Kenya kuanzia 1978 hado 2002, ambapo katika muda huo alitambulika kama karakana ya michezo duniani katika mashindano ya riadha na michezo mingine.

Alichangia katika ufanisi wa Kenya uliopatikana katika riadha, voliboli, ushindi wa Gor Mahia katika gozi la Mandela Cup mnamo 1987, miongoni mwa michezo mingine.

Kama mwanamichezo aliyechezea timu ya Bunge FC miaka ya sitini, Moi alihakikisha kuwa wanamichezo nchini wanajiandalia katika mazingara bora hasa miaka ya themanini, mara tu alipochukua usukani.

Kulingana na aliyekuwa msimamizi wa idara yake ya habari, Lee Njiru, marehemu aliamini katika lishe bora na kufanya mazoezi ya kumfanya awe imara daima.

Mara kwa mara alifanya mazoezi ya viungo. Lakini umri ulivyozidi kusonga, marehemu Moi aliyekufa wiki jana akiwa na umri wa miaka 95, alitumia wakati wake kuhudhuria mechi mbalimbali za kimataifa viwanjani.

Kadhalika alipendelea kushuhudia mashindano ya Moi Golden Cup (sasa SportPesa Shield), ambayo mshindi huwakilisha taifa katika dimba la Confederations Cup, barani Afrika.

Marehemu alikuwa mfano mwema kwa wanamichezo wengi waliomsalimia viwanjani kabla ya mechi kuanza, alipokuwa mgeni wa heshima kwenye fainali nyingi za ubingwa wa kitaifa na kutoa vikombe vya ushindi kwa washindi.

Mbali na kuwa shabiki nambari moja, Moi pia alichangia katika maamuzi mbalimbali ambayo yalinyoosha uongozi wa michezo nchini.

Ni wakati wake ambapo mashirika ya serikali kama Kenya Railways, Kenya Prisons, Kenya Pipeline, Posta, Ministry of Works (MOW), Eldoret KCC, Kenya Ports Authority na Rivatex yalidhamini michezo na kuwaajiri wanamichezo wengi.

Hadi sasa, timu za Kenya Prisons na Kenya Pipeline zimeendelea kuwa hodari katika voliboli katika kiwango cha kimataifa.

Aliambia wachezaji umuhimu wa kufaulu katika ngazi ya kitaifa na kuwaalika Ikulu mara kwa mara baada ya kutwaa mataji mbalimbali ya kimataifa kuwapongeza mwenyewe na kutoa zawadi kwa wachezaji.

Timu kubwa nchini, Gor Mahia na AFC Leopards ziliwahi kupata ardhi za kujenga viwanja kutoka kwa marehemu.

Mwanariadha jagina, Kipchoge Keino anaeleza kujengwa kwa viwanja hivi kuliiwezesha Kenya kupiga hatua kubwa michezoni, mbali na kupata fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa, pamoja na kuimarisha vipaji vya wanamichezo nchini.