Habari Mseto

Huenda pasta aachiliwe huru kuhusiana na kesi ya ubakaji

April 2nd, 2019 2 min read

LUCY MKANYIKA na BRIAN OCHRO

MAHAKAMA ya Voi huenda yakatupilia mbali kesi ya unajisi dhidi ya mhubiri mmoja wa eneo hilo baada ya msichana anayedaiwa kudhulumiwa kutoweka.

Kiongozi wa mashtaka katika kesi hiyo Bi Grace Mkangu aliomba mahakama kumwondolea Bw Boniface Mwasi shtaka hilo hadi pale mlalamishi atakapopatikana.

Bi Mkangu alisema kuwa mchunguzi wa kesi hiyo anaendelea na kumsaka msichana huyo.

“Punde tu tutakapompata mlalamishi tutaendelea na kesi,” akasema.

Hakimu Mkazi wa mahakama hayo, Bw Benerd Onkoba alisema kuwa atatoa uamuzi wake baada ya wiki mbili.

Alimtaka kiongozi wa mashtaka kuwasilisha mahakamani ripoti ya uchunguzi kutoka kwa idara ya uchunguzi.

“Nitatoa uamuzi nikipata ripoti hiyo,” akasema. Msichana huyo alidai kuwa alikuwa amenajisiwa na kupachikwa mimba na pasta huyo miaka miwili iliyopita.

Kabla ya kutoweka, mlalamishi ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili alikuwa mjamzito wa miezi nne.

Alitoweka alipokuwa amehudhuria kesi hiyo mnamo Aprili 28, 2017 katika mahakama ya Voi. Kesi hiyo imetajwa zaidi ya mara 17 bila mlalamishi kuwepo.

Familia yake ilieleza kutoridhika kwao na kuvitaka vyombo husika kuwasaidia kupata mwana wao.

Wakati huohuo, polisi mjini Voi wanamzuilia afisa mmoja wa kaunti kwa madai ya kumnajisi mtoto wa miaka saba.

Mwanamme huyo alikamatwa baada ya mtoto huyo wa darasa la nne kudai kuwa alikuwa amemnajisi nyumbani kwake.

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Voi Bw Joseph Chesire alisema kuwa mshukiwa atafikishwa mahakamani mnamo Jumatano.

“Tunaendelea na uchunguzi ili kupata ushahidi kamili wa kesi hii,” akasema. Alisema kuwa mshukiwa ni jirani ya mtoto aliyenajisiwa.

Kaunti hiyo inaongoza nchini kwa kesi za dhuluma za kijinsia kama vile ulawiti, ubakaji na unajisi.

Katika mahakama ya Mombasa, mfanyabiashara aliyehukumiwa miaka 22 kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini ya thamani ya Sh30 milioni alinyimwa dhamana.

Ahmed Said Bakari alikata rufaa kifungo na alikuwa ameomba mahakama imuachilie kwa dhamana huku akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa hiyo.

Jaji Njoki Mwangi alisema hakuridhishwa na sababu za mshtakiwa kutaka dhamana.

Kando na kifungo cha miaka 22, Bw Bakari pia alitozwa faini ya Sh8 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya ambazo zilidaiwa zilikuwa zinasafirishwa Madagascar.

Katika karatasi yake ya rufaa, mshukiwa huyo anasema kuwa alifungwa kwa mashtaka ambayo hayakuandikwa kwa njia inayofaa na kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hayakuwa ya ukweli.

Pia, anaongezea kuwa alifungwa jela kwa tuhuma tu, ambayo haikuthibitishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

Bw Bakari hata hivyo, anataka Mahakama ya Rufaa kufutilia mbali hukumu hiyo ya mahakama ya hakimu.

Mshukiwa huyo alikuwa amefungwa pamoja na raia wa Seychelles Clement Serge Bristol, ambaye alihukumiwa miaka 10 na kutozwa faini ya ziada ya Sh5 milioni.