Habari Mseto

Huenda shule 50 zikafungwa kutokana na ukame

February 11th, 2019 1 min read

 Na FLORAH KOECH

SHULE za msingi zaidi ya 50 katika Kaunti ya Baringo huenda zikafungwa kutokana na ukosefu wa maji uliosababishwa na ukame wa muda mrefu.

Shule zilizoathiriwa zaidi na ukame ni Nasorot, Toplen, Naudo, Lochokia, Napukut, Kang’uria, Silale, Korelach, Katagh, Embositit, Kapunyany, Chemayes, Ptikii , Riong’o, Akwichatis, Chesakam na Nakule.

Shule nyingine ambazo huenda zikafungwa ni Cheptaran, Nalekat, Cheptunoiyo, Natan Orusion, Nasorot, Akule, Toplen, Silale, Napeikore, Nalekat, Napukut, Kitailem, Cheptamas, Kangoria, Nakoko, Cheptunoyo, Lotita, Chemisik, Kositei, katikit, Chemoliongot na Chemukutan, zote katika eneo la Tiaty.

Katika eneobunge la Baringo Kaskazini kunaTorolokwonin, Kipchar, Oinobkoloswo, Kaptigit, Chesangich, Kapero, Kuikui, Ayatya, Torolokwonin, Barwessa, Marigut, Kinyach Ngaratuko, Chemoe, Yatya, Tuluk, Kagir, Loruk, Chepkesin, Kapturo, Toboroi, Barsuswo na Lokorotabim.

Katika eneo la Baringo Kusini ni Ramacha, Karma, Katilimwo, Kapindasum, Chemorongion, Embosos, Arabal, Chebinyiny, Sosionte, Nyimbei, Kasiela, Keon, Tuiyotich, Rugus, Noosukro na Sirata.

Kulingana na mkuu wa shule ya Chesakam, Patrick Mudanya, mito yote ambapo walikuwa wakiteka maji ya kunywa na kupikia imekauka.

“Kuna hofu kuwa shule nyingi, haswa katika eneobunge la Tiaty zitafungwa kutokana na uhaba wa maji. Hali huenda ikawa mbaya zaidi iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa shule zinapata maji,” akasema Bw Mudanya.

Kulingana na wakazi, mito waliyokuwa wakitegemea kama vile Nginyang’ Akwichatis, Kositei, Kasitit, Chemsik, Kaptobokwo na Mukur tayari imekauka.

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo wanatumia muda mwingi wakitafuta maji badala ya kujihusisha na shughuli za maendeleo kama vile kilimo na elimu.

Kulingana na mkazi wa kijiji cha Akwichatis, Lourien Lomariwa, ukame huo umelazimu wengi wa wakazi wa eneo hilo kuhamia katika maeneo mengine kutafuta malisho na maji ya mifugo wao.

Alisema wanafunzi wanakosa kwenda shuleni kwa sababu wanawasaidia wazazi wao kutafuta maji.