Habari Mseto

'Huenda uhaba wa chakula muhimu ukaanza kushuhudiwa'

May 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Kilimo imeonya huenda upungufu wa chakula muhimu ukaanza kushuhudiwa hivi karibuni kufuatia mzozo wa maeneo ya mpakani baina ya Kenya na Tanzania.

Kulingana na wizara, bei za mahindi, mboga na matunda zinatarajiwa kupanda maradufu.

Onyo hilo limejiri licha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuahidi kutatua mzozo uliopo.

Rais Kenyatta mnamo Jumamosi alitangaza kufunga mipaka ya Kenya na Tanzania na vilevile Somalia, kutokana na ongezeko la visa vya Covid – 19 maeneo ya mipakani, ila malori ya mizigo pekee kuruhusiwa kuingia.

Amri hiyo aidha imezua tumbojoto kati ya mataifa haya mawili.

Akiahidi mzozano uliopo unaendelea kutatuliwa, Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema Jumatano changamoto zinazidi kuibuka kuingiza chakula nchini.

“Shida iliyopo tunaendelea kuitatua. Hakika, kuna ugumu kuingiza chakula nchini,” waziri akasema.

Rais wa Tanzania Dkt Magufuli alinukuliwa Jumatano akisema Kenya na taifa lake ni ndugu, na mzozo uliojiri unasuluhishwa, akieleza kwamba athari za Covid-19 hazipaswi kusambaratisha usahibu wa mataifa haya mawili.

Sasa waziri Munya anahimiza wakulima wa Kenya kujibidiisha kuzalisha chakula.

“Hii ni fursa ya wakulima wetu kuweka bidii katika shughuli za kilimo,” waziri akasema.

Tanzania ni mzalishaji mkuu wa nafaka, mboga, nyanya, vitunguu, matunda, na mazao mengine, mengi yanayouzwa Nairobi na viunga vyake.

Uhaba wa chakula ni miongoni mwa athari zilizosababishwa na janga la Covid-19.