Habari

'Huenda ukalazimika kupimwa Covid-19 kabla ulazwe hospitalini'

May 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HUENDA Wakenya wote watakaohitajika kulazwa hospitalini kwa matibabu zaidi wakalazimika kupimwa kubaini kama wana virusi vya corona kabla ya kuhudumiwa, ikiwa pendekezo jipya la Wizara ya Afya litaidhinishwa.

Akiongea Jumatatu nje ya makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya Dkt Patrick Amoth amesema hatua hiyo inalenga kuwakinga wahudumu wa afya na wagonjwa waliolazwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba ikiwa mgonjwa wa Covid-19 asiyedhihirisha dalili atalazwa hospitalini, anaweza akawaambukiza wagonjwa wengine au hata wahudumu wa afya. Utaratibu huu mpya unalenga kuwalinda watu kama hawa,” Dkt Amoth akasema.

Amesema utaratibu huo mpya huenda ukaanza kutekelezwa baada ya kuchambuliwa upya kwa miongozo inayotumiwa na wataalamu wa afya kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19.

“Baada miongozo hiyo kupigwa msasa, tutahitaji kwamba Wakenya wote wanaosaka huduma za afya kutoka hospitali za serikali wapimwe virusi vya corona kwanza kabla ya wao kulazwa,” akaeleza Dkt Amoth.

“Kabla ya kukubaliwa kulazwa hospitalini, mojawapo ya vipimo ambavyo utafanyiwa ni cha Covid-19. Hii itawakinga wahudumu wa afya na wagonjwa wengine ambao huenda wakaathiriwa,” akaongeza.

Wakati huo huo, Dkt Amoth amesema Wizara ya Afya inaendeleza mpango wa kusambaza vyombo vya kupimia Covid-19 katika hospitali zote za umma ili kuhakikisha kuwa Wakenya hawatakosa kutibiwa kwa misingi ya kutopimwa kubaini kama wana virusi vya corona au la.

“Hivi vipimio (test kits) vitasambazwa kwa utaratibu utakaohakikisha kuwa Wakenya hawatanyimwa huduma za afya katika hospitali yoyote kwa misingi kwamba hawajapimwa virusi vya corona,” akaeleza.

Kufikia Jumatatu, Kenya imekuwa imeandikisha jumla ya visa 700 vya maambukizi ya Covid-19 baada ya watu 28 zaidi kubainika ni wagonjwa.

Miongoni mwa wagonjwa hao wapya ni madereva tisa raia wa Kenya ambao waliingia nchini kutoka Tanzania kupitia mpaka wa Namanga.