Michezo

Huenda Victor Wanyama akaondoka Spurs

June 14th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya Mkenya Victor Wanyama kumaliza kandarasi yake na Tottenham Hotspur mnamo Juni 30 mwaka 2021 yanazidi kuwa finyu baada ya vyombo vya habari nchini Uingereza kudai kwamba huenda asiwe katika orodha ya wachezaji wa klabu hii msimu ujao wa 2019-2020.

Mashirika mbalimbali ya habari nchini Uingereza yamesema Ijumaa kwamba Wanyama, ambaye kulingana na tovuti ya Transfermarkt bei yake sokoni ni kati ya Sh2.0 bilioni na Sh2.2 bilioni, atakosa kazi uwanjani Tottenham Hotspur kocha Mauricio Pochettino akifaulu kusaini kiungo Mfaransa Tanguy Ndombele katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho kitakachofungwa Agosti 8 nchini Uingereza.

Wanyama, ambaye atasherehekea miaka 28 ya kuzaliwa kwake hapo Juni 25, amekuwa akihusishwa na uhamisho tangu aanze kusumbuliwa na majeraha msimu 2017-2018.

Msimu 2018-2019, alichezea Spurs mechi 22 (13 kwenye Ligi Kuu, 6 katika Klabu Bingwa Ulaya, 2 kwenye League Cup na 1 katika Kombe la FA) kati ya 58 klabu hiyo ilisakata katika mashindano yote.

Tangu aungane na kocha wake wa zamani Mauricio Pochettino katika klabu ya Spurs mnamo Julai 1 mwaka 2016, nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya amekuwa mkekani siku 232 zikiwemo siku 133 msimu 2017-2018 kwa kuchanika misuli na siku 99 akiuguza majeraha ya magoti msimu 2018-2019.

Historia hii ya majeraha imefanya aonekane kuwa mzigo kwa Spurs ambayo sasa inamezea mate kiungo wa Lyon, Ndombele aliyeng’ara sana katika Klabu Bingwa msimu 2018-2019.

Inasemekana Spurs tayari imeanzisha mazungumzo na Ndombele, ambaye asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na imejawa na imani itamnyakua.

Lyon imeweka bei ya mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 22 kuwa Sh9.1 bilioni, bei ambayo huenda ikawa kikwazo katika uhamisho wake.

Wanyama aliwahi kuhusishwa na uhamisho hadi Manchester United, Liverpool (Uingereza) na AS Roma (Italia) miezi iliyoenda, lakini itakuwa vigumu kwake kuelekea huko kutokana na rekodi mbovu ya majeraha, licha ya kuwa yeye huwa na bidii anapokuwa katika hali nzuri.

Mchezaji huyu wa zamani wa Nairobi City Stars, AFC Leopards (Kenya), Helsingborg (Uswidi), Germinal Beerschot (Ubelgiji), Celtic (Scotland) na Southampton (Uingereza) yuko nchini Ufaransa katika kambi ya mazoezi ya Harambee Stars inayojiandaa kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Misri kutoka Juni 21 hadi Julai 19 mwaka 2019.

Afunga bao

Alifungia Kenya bao, kupitia penalti, lililozamisha Madagascar katika mechi ya kirafiki jijini Paris mnamo Juni 7.

Anatarajiwa kutumiwa japo kidogo katika mechi ya pili na mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya DR Congo jijini Madrid nchini Uhispania mnamo Juni 15.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wataelekea Madrid mapema Juni 15 na kulimana na DR Congo baadaye Juni 15 usiku. Wataelekea nchini Misri mnamo Juni 19 kumenyana na Senegal, Algeria na Tanzania katika Kundi C.