HabariSiasa

Huenda Waiguru akang'olewa mamlakani

April 1st, 2020 2 min read

NA GEORGE MUNENE

GAVANA wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru huenda akang’atuliwa mamlakani baada ya notisi ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake kufikishwa katika bunge la kaunti hiyo Jumatano.

Mswada huo uliwasilishwa na diwani wa Mutira Bw Kinyua Wangui ambaye alimshutumu gavana huyo kwa kuvunja sheria za Katiba.

Gavana huyo amekejeliwa kwa kuenda kinyume na sharia kwa kudinda kutoa hotuba ya kila mwaka kwa bunge la kaunti hiyo, kitendo ambacho Bw Wangui alisema kilivunja sheria za serikali kuu na kaunti.

Bw Wangui pia alikasirishwa na gavana huyo kwa kuvunja Sheria ya Utoaji wa Kandarasi na Uzoaji wa Mali kwa kudhalilisha mamlaka ya afisa wa uhasibu, kwa kuunda kamati ya kupitisha zabuni iliyojaa ‘wafanyakazi wake’ kwa manufaa yake mwenyewe.

Bi Waiguru pia amejipata matatani kwa kutumia afisi yake kujilipa Sh10.6 milioni kama marupurupu ya usafiri ilhali hakusafiri popote.

Bunge la kaunti liliambiwa gavana huyo pia alikuwa anawapa kandarasi marafiki zake na kampuni anazohusika nazo.

“Inashangaza sana baadhi ya kandarasi zilipewa kampuni inayohusishwa na afisa mmoja katika serikali ya Bi Waiguru,” akasema Bw Wangui.

Kabla ya kwasilishwa kwa mswada huo, gavana huyo alifokea wawakilishi wa wadi kwa kupanga njama ya kumtoa mamlakani.

Aliwataka madiwani hao kukoma kuangazia mambo yasiyo na maana badala ya kuangazia vita dhidi ya virusi vya corona

“Inasitikisha sana wakati taifa la Kenya na dunia nzima inapambana na janga la virusi vya corona mawakilishi wa wadi wengine wanangazia mambo ya kisiasa yasiyo na maana na mswada wa kunitoa mamlakani usiokuwa na misingi,” alisema Bi Waiguru.

Bi Waiguru alijitetea dhidi ya habari kwamba amekuwa akifaidika na kandarasi za serikali.

“Hizi ni propaganda za kujitafutia umaarufu.”

Wawakilishi wadi hao pia wanamshutumu Bi Waiguru kwa kujinunulia gari la Sh15 milioni bila kufuata sheria za kandarasi.

Alielezea kuwa alinunua magari hayo kulingana na sheria za kandarasi za serikali zinazowiana na zile za Wizara ya Kazi za Umma na “hayo si matumizi mabaya ya pesa za umma.”

“Madiwani hawa wanapaswa kusoma na kuelewa maana ya utumizi mbaya wa pesa za umma kabla ya kunishutumu kwa ubadhirifu wa pesa,” alijitetea.

Alipuuzilia mbali madai kwamba kuwa sekta ya afya iko katika hali mbaya karika kaunti hiyo.

Alidai kuwa mswada huo wa kumtoa mamlakani umefikishwa bungeni kwa sababu alikataa kuwapa kandarasi madiwani hao.

IMETAFSIRIWA NA FAUSTINE NGILA