Habari Mseto

Huenda wanaraga wakatupwa ndani miaka 15 kwa ubakaji

July 9th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WACHEZAJI wa raga Frank Wanyama na Alex Mahaga wanaokabiliwa na shtaka la ubakaji watajua hatima yao Alhamisi uamuzi utakaposomwa.

Endapo watapatikana na hatia huenda wakasukumwa jela kifungo cha miaka 15.

Hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku aliwaomba msamaha washukiwa hao pamoja na wakili wao Bw Wafula Simiyu kwa kutousoma uamuzi wa kesi hiyo kama alivyokuwa amesema mwezi uliopita.

“Samahani, uamuzi wa kesi dhidi ya Wanyama na Mahaga hauko tayari kama nilivyokuwa nimesema mwezi uliopita. Shughuli za mahakama zimekuwa nyingi na sikuweza kufanikiwa kuuandaa. Samahani,” Bi Mutuku aliwaeleza.

Hakimu huyo aliwaambia washtakiwa hao atausoma uamuzi huo Julai 11, 2019.

Wachezaji hao wa timu ya Kenya Harlequin RFC walikanusha shtaka la kumbaka mwanafuzi kwa zamu mnamo Februari 10 miaka miwili iliyopita. Wawili hao walifanyiwa ukaguzi wa DNA.

Mawakili Wafula Simiyu na Ombui Ratemo walieleza mahakama mlalamishi hakulazimishwa kushiriki ngono na wawili hao.

Lakini kiongozi wa mashtaka Everlyne Onuga alipinga ushahidi huo wa washtakiwa na kusema walimbaka.