Huenda wandani wa Ruto Kisii wakamtoroka hivi karibuni

Huenda wandani wa Ruto Kisii wakamtoroka hivi karibuni

Na RUTH MBULA

WABUNGE kadhaa ambao wamekuwa wakimuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wameashiria uwezekano wao kumhepa wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Wabunge hao wa mrengo wa Tangatanga kutoka jamii ya Gusii, wamedokeza kuwa, endapo Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, atatangaza wazi nia yake kuwania urais 2022, basi hawatakuwa na budi kubadili mkondo wa kisiasa.

Mbunge wa Mugirango Kaskazini, Bw Joash Nyamoko, mwenzake wa Kitutu Masaba, Shadrack Mose na Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi), ambao wanatoka kaunti Nyamira, nyumbani kwa Dkt Matiang’i, hivi majuzi walisema watafanya kazi pamoja na waziri huyo hata wanapoendelea kushirikiana na Dkt Ruto.Tangazo la wabunge hao liliwakanganya wafuasi wao na baadhi ya wakazi.

Wanasiasa wandani wa Dkt Matiang’i, wanasema atatangaza mwelekeo wake wa kisiasa hivi karibuni na kwamba tangazo la wabunge wa Tangatanga linalenga kuhakikisha kuwa “hawaachwi nje” ya mipango ya waziri huyo.

Wakazi wanahisi hatua ya wabunge hao itavuruga juhudi za Dkt Ruto za kujinadi katika kaunti ya Nyamira na eneo la Gusii kwa jumla. Wabunge hao watatu walitoa tangazo hilo katika ibada ya mazishi katika kijiji cha Tinga, ambayo pia ilihudhuriwa na Dkt Matiang’i.

“Ndio ningetaka kumwambia Waziri kwamba niko nyuma yake kikamilifu. Mtu asimdanganye kwamba sisi ni maadui wake kwani hatuoni haja ya kumpiga vita. Hatuwezi kwenda kinyume na matakwa ya watu wetu,” akasema Bw Nyamoko.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Mbunge huyo alisema ikiwa Dkt Matiang’i atajitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais, watatoa msimamo wao baada ya tangazo hilo.

Alilalamika kuwa jamii ya Abagusi imekuwa ikidharauliwa na jamii zingine kutokana na ukosefu wa umoja miongoni mwa viongozi wake.

Bw Nyamoko alisema kila jamii nchini ina kiongozi wake ambaye hutetea maslahi yake katika ngazi ya kitaifa lakini jamii ya Gusii hutumiwa kujazia hesabu ilhali haijaitisha mgao wake katika meza ya kitaifa.

“Ukienda magharibi mwa Kenya, kuna Mudavadi, Wetang’ula na Oparanya wanaowakilisha maslahi ya Waluhya, Ukienda Ukambani, kuna Kalonzo Musyoka. Eneo la Mlima Kenya linawakilishwa na Rais Uhuru Kenyatta ilhali Rift Valley iko nyuma ya Ruto. Nani anawakilisha eneo la Gusii?” akauliza mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza.

Bw Nyamoko aliongeza kuwa wanaunga mkono mipango ya kumtawaza Dkt Matiang’i kama msemaji wa jamii ya Abagusii.

“Tunahitaji mtu ambaye tutamtegemea katika masuala ya kijamii. Waziri huyo mwenye bidii anahitaji nafasi hiyo,” akasema Nyamoko.Tangazo la watatu hao linajiri miezi michache baada ya Naibu Gavana wa Kisii, mfuasi mkuu wa Dkt Ruto katika kaunti ya Kisii, kutangaza kuwa atafanyakazi na Dkt Matiang’i kuimarisha umoja wa jamii ya Abagusii.

You can share this post!

Raila amtetea Ruto

NLC yataka maskwota wa tangu ukoloni sasa wapewe makao