Michezo

Huenda Zidane atue Juve, Chelsea kula hu

February 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Chelsea inaonekana itaambulia pakavu katika juhudi zake za kuajiri Zinedine Zidane.

Chelsea, ambayo imetimua makocha 11 katika kipindi cha miaka 14, inasemekana inamezea mate Mfaransa huyu.

Zidane alipata sifa kubwa kama kocha alipoongoza miamba wa Uhispania Real Madrid kutwaa mataji matatu ya Klabu Bingwa Ulaya katika misimu mitatu aliyoiongoza kabla ya kujiuzulu Mei 31, 2018.

Chelsea inasemekana itapiga kalamu Maurizio Sarri akipoteza mojawapo ya mechi tatu zijazo – dhidi ya Malmo (Ligi ya Uropa), Manchester City (League Cup) na Tottenham Hotspur (Ligi Kuu) – zitakazosakatwa Februari 21, Februari 24 na Februari 27 uwanjani Stamford Bridge.

Sarri ameapa kupigania wadhifa wake kwa kupata matokeo mazuri. Hata hivyo, mashabiki wana sauti moja kwamba hawamtaki na wameishauri Chelsea imtafute Zidane.

Hata hivyo, ripoti zinadai kwamba Zidane anamezea mate Juventus, ambayo tetesi zinasema inapanga kutengana na Massimiliano Allegri kwa sababu ya ukame wa mataji ya Klabu Bingwa Ulaya.