Habari Mseto

Hujuma polisi kuacha jeneza barabarani

June 1st, 2020 1 min read

NA DAVID MUCHUI

KAUNTI ya Meru imekejeliwa kwa kile wakazi wanasema ni kuwahujumu waombolezaji, katika juhudi zake za kuhakikisha kanuni za kudhibiti virusi vya corona zimefuatwa. 

Hii ni baada ya polisi na maafisa wa afya kuwazuia waombolezaji kutoka Malinda hapo Alhamisi kuingia katika kaunti hiyo katika mpaka wa Meru na Tharaka Nithi.

Bw Charles Mwenda, ambaye alimpoteza mkewe aliyefariki kutokana na kansa, aliwalaumu maafisa hao kwa kuwadhulumu waombolezaji.

Lakini Mshirikishi wa kaunti hiyo Allan Machari alisema Bw Mwenda alisaidiwa kusafirisha maiti ya mkewe kwa mazishi baada ya basi walilotumia kutoka Malindi kuzuiliwa.

Bw Mwenda alilalama kuwa waombolezaji hao walikatazwa kusafiri hadi nyumbani kwa mazishi licha ya vipimo vya vya Covid-19 kuonyesha hawakuwa na virusi hivyo.

“Tulifika katika eneo la mpaka la Keeria saa tano usiku Alhamisi ambapo polisi walisimamisha basi letu na kuamrisha abiria wote kutoka kwa basi. Baada ya mazungumzo marefu, familia yangu na marafiki walilazimika kurudi Malindi. Niliachwa peke yangu na jeneza iliyowekwa kwa gari la polisi,” Mwenda aliambia Taifa Leo.

Alisema kuwa maafisa hao walimwacha pamoja na jeneza hilo katika Kituo cha Polisi cha Kianjai ambapo alilala usiku huo kabla ya rafiki yako kumkujia siku iliyofuata.

“Mwili wa mke wangu ulitolewa kwa gari la polisi na kuwekwa barabarani. Walikataa kunipeleka nyumbani kilomita tano kutoka Kianjai. Kwa kuwa kulikuwa kunanyesha, nililazimika kuweka jeneza hilo chini ya lori lililoegeshwa hapo,” alisimulia.