HUKU USWAHILINI: Biashara kwetu zina raha zake

HUKU USWAHILINI: Biashara kwetu zina raha zake

Na SIZARINA HAMISI

BINAFSI, nimezaliwa katika familia ya akina dada wa kutosha.

Binti azizi mmoja, dada wanne, mama mmoja, nyanya wawili na shangazi wasiohesabika.

Wote hawa wamenipa fursa na nafasi ya kuwajua na kuwasherehekea wanawake katika maisha ya kila siku.

Licha ya ufanisi wa kielimu, kimaisha, kisiasa, kiuchumi ambao kizazi hiki cha hawa kimefaulu kupata, bado hawajapoteza uanamke wao.

Bado hawana kiburi ama patashika lukuki nilizowahi kukutana nazo kwa wanawake wa hulka mbalimbali.

Kila mwanamke ana haki ya kuwa mwanamke na si kujaribu kuiga wanaume ambao anakutana nao sehemu za pilkapilka za maisha kila siku.

Kwa jinsi wanawake wengi walivyo wapiganaji wa maisha huku Uswahilini, kumekuwa na taswira pamoja na mtizamo kwamba kile ambacho mwanaume anaweza kufanya, mwanamke anaweza kufanya bora zaidi.

Ukitaka kujua mapambano ya maisha ya wanawake wa Uswahilini, angalia shughuli zao tangu wanapoamka asubuhi. Mitaa yetu asubuhi huwa hakuna shida ya kitafunwa kwa kifungua kinywa, kwani ni chaguo lako.

Mtaa huwa umepangwa biashara za masinia ya vitumbua, mahamri, chapati hadi supu ya matumbo.

Wafanyabiashara hawa wa asubuhi ni wanawake ambao hujidamka kuweza kuuza chochote kupata pesa za mahitaji ya familia.

Halikadhalika, muda wa jioni, biashara hurudi tena barabarani na wakati huu akina dada hujipanga na masufuria ya wali, maharagwe, mchuzi wa nyama na hata uji wa mchele ili kupata riziki zao.

Haya yote hufanywa kwa juhudi kubwa na wakati mwingine bila usaidizi wa mwanaume.

Na wadada wa Uswahilini wanajua kuvutia wateja katika biashara zao, kawaida maneno yao kwa wateja huwa ni ya faraja na kusuuza moyo, kushauri na wakati mwingine kuelekeza na kuongoza.

Wapo wanaoenda kununua chakula kwa wanawake hawa kwa ajili ya kupata maneno ambayo huwaletea faraja.

Pamoja na hawa wenye maneno ya busara wapo pia wenye maneno ya kuchamba, ambao pia wana wateja wao.

Akina dada hawa huwa na mashabiki wengi huku kwetu, kwani wengi wanaoenda kununua bidhaa zao hupata na habari zote zinazoendelea mtaani.

Kuanzia yule aliyepigwa na kuachiwa jeraha na mumewe, mwanamke aliyemfumania mumewe na mwanamke wa jirani, jirani mlevi alivyorudi nyumbani akiwa amevaa suruali kichwani na hata yule msichana ambaye shughuli zake hazieleweki mtaani.

Biashara zetu huku Uswahilini pia zina raha zake.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

Cherono aibuka mfalme mpya wa Valencia Marathon

FATAKI: Ni upumbavu kuamini thamani ya mwanamke hushuka...

T L