Habari za Kitaifa

Hukumu dhidi ya Maribe, Jowie yaahirishwa hadi Machi 15

January 26th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

HUKUMU ya kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani inayowakabili waliokuwa wapenzi Joseph Irungu almaarufu Jowie na mtangazaji Jacque Maribe, imeahirishwa hadi Machi 15, 2024, kufuatia kuugua kwa mwanahabari huyo.

Jaji Grace Nzioka alipokuwa akijitayarisha kusoma hukumu Ijumaa, mwanahabari huyo hakujitokeza.

Wakili Katwa Kigen ameambia mahakama kwamba mteja wake hajihisi vizuri ingawa “alikuwa tayari kwa hukumu”.

Upande wa mashtaka na wakili wa Jowie, hawakupinga wasilisho mahakamani kwamba kikao cha hukumu kiahirishwe.

Maribe na Jowie walishtakiwa kwa mauaji ya Monicah mnamo Septemba 2018.

Jaji Nzioka alitwaa usukani wa kusikiliza kesi hiyo kutoka kwa Jaji James Wakiaga aliyehamishwa kutoka kitengo cha kusikiliza kesi za mauaji hadi kuamua kesi za biashara.

Wawili hao walishtakiwa mnamo Oktoba 2018 na kuzuiliwa katika magereza ya Industrial Area (Jowie) na Lang’ata (Maribe).

Mahakama ilimwachilia Maribe kwa dhamana lakini Jowie akanyimwa hadi pale mashahidi fulani waliodai walihofia maisha yao akiachiliwa kwa dhamana, walipokamilisha kutoa ushahidi.

Maiti ya Monicah ilipatikana ndani ya bafu katika mtaa wa Kilimani.

Mikono ilikuwa imefungwa na shingo kukatwa kwa kisu.

Maji ya mfereji katika bafu ya Monicah yalikuwa yamefunguliwa.

Mashahidi waliofika kortini, walieleza mahakama Jowie ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuonekana na Monicah.

Ushahidi mwingine uliotolewa ni kwamba Jowie alitumia gari la Maribe kuenda katika makazi ya Monicah usiku alipouawa.

Akiwa mtangazaji katika kituo cha televisheni, Maribe ndiye alipeperusha habari za mauaji ya Monicah.

Jaji Nzioka alielezwa kwamba Jowie alikuwa ameomba bastola ya jirani ya Maribe.

Lakini wote walijitenga na mauaji hayo wakisema hawakuhusika kamwe.

Alipokumbana na mauti, Monicah alikuwa ametua Nairobi kutoka Sudan Kusini ambako alikuwa akifanya biashara.

Maelezo zaidi na Sam Kiplagat