Habari za Kitaifa

Hukumu ya ajabu padri mnajisi akipewa kifungo cha kuhubiri dhidi ya dhuluma za kimapenzi

April 3rd, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

PADRE wa Kanisa Katoliki mjini Mombasa aliyepatikana na hatia ya kumdhulumu kingono msichana mwenye umri wa miaka 16, amepewa adhabu ya kifungo cha nje ambapo anahitajika kuwaelimisha waumini wake kuhusu Sheria ya Makosa ya Dhuluma za Kingono.

Mahakama Kuu mjini Mombasa ilifutilia mbali adhabu kali ya kifungo cha miaka saba jela ambayo Padre Dominic Muli Nzioka alikuwa amepewa na Mahakama ya Hakimu.

Badala yake, sasa ameachwa aende akahubiri injili ya dhuluma za kingono angalau mara moja kwa mwezi, siku ya Jumapili kwa miaka mitatu ambayo atakuwa akitumikia kifungo cha nje.

Haya yatafuatiliwa kwa karibu na Askofu wa Parokia na afisa wa kuchunguza tabia, ambao wanatakiwa kuthibitisha utekelezaji wa jukumu hilo hadi muda wake utakapoisha.

Jaji Anne Ongi’injo alikubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu kuwa, upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote.

“Hata hivyo, Mahakama hii imefutilia mbali kifungo cha miaka saba gerezani,” Jaji Ong’injo alisema.

Jaji huyo alibaini kuwa, Bw Nzioka alitumia nafasi ya kuwa mlezi wa kiroho kwa mtoto huyo kumtia moyo kumkaidi mzazi wake, kinyume cha amri 10 ambazo anapaswa kuzishika na kuzilinda.

Mshtakiwa alikuwa amepatwa na hatia mwaka uliopita lakini akakata rufaa.

Mahakama ya Hakimu ilimpata na hatia kwa kosa alilotenda mnamo Septemba 28, 2020, katika eneo la Mtopanga, Kaunti Ndogo ya Kisauni.

Mahakama ilielezwa kuwa, mnamo Septemba 28, 2020, mshtakiwa alimtumia mtoto huyo ujumbe kwenye simu yake na kumuagiza aende kanisani.

Alipofika, alienda kwenye moja ya nyumba za parokia. Mwanaume aliyekuwa na Padri huyo aliondoka na kuwaacha wawili hao.

“Padri Dominic alikuwa na pombe ambayo alininywesha. Kisha akanigusa isivyostahili,” mtoto huyo alieleza alipokuwa akitoa ushahidi mahakamani.

Pia, alisema hakuwa na sababu ya kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya mshtakiwa.

Mama wa mtoto huyo aliithibitishia mahakama kuwa, alimuonya Bw Nzioka dhidi ya kuandikiana jumbe na mtoto wake. Alidai kuwa, kiongozi huyo wa dini alimtembelea mtoto wake nyumbani kwake mara mbili bila yeye kujua.

Uchunguzi wa kimatibabu uliofanyiwa mtoto huyo hata hivyo ulionyesha kuwa hakunajisiwa. Kwa upande wake, mshtakiwa alikanusha kosa hilo lakini alikiri kukutana na kumpa mtoto huyo kinywaji.

Alieleza mahakama kuwa, mtoto huyo alilalmikia hali ngumu ya masomo ya mtandaoni aliyokuwa nayo katika kipindi cha Covid-19.

‘Nilimhakikishia kuwa serikali itafungua tena shule na ataendelea na masomo. Nilimtia moyo awe mvumilivu,” aliambia mahakama.

Pia, alikanusha kupokea simu zozote kutoka kwa mamake mwathiriwa lakini alikiri kwamba, mwanamke huyo hapo awali alimpigia simu na kumuonya dhidi ya kuandikiana jumbe na kuongea na mtoto huyo.

Inasemekana kwamba, alimwambia mama wa mwathiriwa kuwa yeye ni mshauri na lilikuwa chaguo la mtoto kuenda kwake kwani alijisikia huru kuzungumza naye kuhusu masuala yake ya kibinafsi.