HUSSEIN HASSAN: Kenya kwenye mtihani mwingine wa kura leo

HUSSEIN HASSAN: Kenya kwenye mtihani mwingine wa kura leo

NA HUSSEIN HASSAN

WANANCHI wa Kenya leo wanaelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kuwachagua viongozi watakaowawakilisha na kusimamia masuala muhimu ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika zoezi hilo la kidemokrasia, wapigakura zaidi ya milioni 22 si tu watakuwa na fursa ya kumchagua rais mpya, lakini pia watawachagua magavana, maseneta na wawakilishi wanawake wa kaunti zote 47 za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wapigakura pia watakuwa na fursa ya kuchagua wabunge 290 na wawakilishi wa wadi (madiwani) 1,450.

Wagombea zaidi ya 18,000 wameidhinishwa kujitosa kwenye mtifuano wa kuwania viti zaidi ya 1,800 vya uwakilishi nchini kote.

Kuna vituo vya kupigia kura zaidi ya 46,000 nchini kote. Hayo ni kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo (IEBC).

Uchaguzi wa mara hii nchini Kenya ni wa aina yake kutokana na sababu mbalimbali.

Tofauti na chaguzi zilizopita, mara hii rais anayeondoka madarakani ametangaza wazi wazi kumuunga mkono kinara wa upinzani.

Rais wa awamu ya pili nchini Kenya, hayati Daniel Toroitich Arap Moi aliingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati Mzee Jomo Kenyatta mwaka 1978.

Mzee Moi aliliongoza taifa kwa miaka 24 tokea kipindi hicho hadi alipostaafu mwaka 2002. Yumkini mapokezano hayo yasingefanyika kiwepesi iwapo mazingira ya wakati huo yangelikuwa ya mvutano kama yanayoshuhudiwa hivi sasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, ambaye anagombea kiti cha rais kupitia chama cha UDA.

Ruto anayeuongoza muungano wa Kenya Kwanza atachuana na kinara wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga, ambaye anaungwa mkono na hata kufanyiwa kampeni na Rais Uhuru Kenyatta.

Mwaka 2002, Uhuru Kenyatta wakati huo bado akiwa mwanagenzi wa siasa, aliteuliwa na Mzee Moi kuwa mgombea wa urais wa chama tawala cha KANU kipindi hicho. Hata hivyo alibwagwa kwa kura nyingi mno na Mwai Kibaki aliyekuwa anapeperusha bendera ya mseto wa vyama vilivyounda muungano wa NARC.

Usuhuba wa Kenyatta na Odinga ulishamiri mwaka 2018, ambapo waliamua kuzika tofauti zao za kisiasa na kimitazamo na kutanguliza mbele maslahi ya taifa.

Baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2017 yaliyokuwa yamempa ushindi Rais Kenyatta aliyegombea kwa muhula wa pili dhidi ya Odinga- ambaye aliwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo.

Uchaguzi wa rais ulirudiwa na Rais Kenyatta akaibuka mshindi tena, lakini taifa bado likawa kwenye hali ya taharuki.

Hapo ndipo Kenyatta na Odinga wakakutana na kufanya mazungumzo ya kina, na kuafikiana kuzika tofauti zao na kuamua kushirikiana katika kile waliochokiita kuwanganisha Wakenya.

Muafaka huo ndio ulikuwa mwanzo wa kusambaratika ndoa ya kisiasa ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto anayeshidana na Raila kwenye kiti cha urais.

Ingawaje tafiti tofauti tofauti za maoni zimeonyesha mwaniaji mmoja kuwa mbele ya mwingine, hicho si kigezo cha kutegemewa bali mwamuzi wa kweli ni mpigakura atayeamua ukweli siku ya leo Agosti 9.

Katika chaguzi za mwaka wa 2013 na 2017, tafiti hizo zilionesha kuwa Odinga alikuwa kifua mbele dhidi ya Kenyatta, lakini mambo yalikuwa tofauti kwa mujibu wa matokeo rasmi ya chaguzi hizo.

Aidha, kwa mujibu wa chunguzi hizo za maoni za hivi karibuni, uwezekano wa uchaguzi wa rais kuingia katika duru ya pili ni mkubwa, kutokana na wagombea hao wawili wakuu kushindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Jamii ya kimataifa imeiweka Kenya kwenye mizani ya kupima iwapo taifa hilo ni kinara tu wa uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati, au pia lina ukomavu wa demokrasia.

Mchambuzi wa masuala ya siasa jijini Nairobi, Prof Makau Mutua anasema: Uchaguzi wa Agosti 9 una umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa Kenya. Taifa lipo katika nukta ya kujitathmini na kujitafakari. Sharti tuukumbatie uchaguzi huu. Wakenya wanaenda kutekeleza haki yao ya msingi huku wakiwajihiwa na changamoto kadhaa, za kiuchumi, kijamii na kiusalama. Taifa hilo, kama mataifa mengine ya dunia, linaendelea kuuguza makovu ya janga la corona na taathira zake hasi, sanjari na kujaribu kujinasua kutoka kwenye matatizo ya kiuchumi, mfumuko wa bei za bidhaa na uhaba wa nafaka uliochangiwa pakubwa na mgogoro wa kivita Ukraine. Vyovyote vile yatakavyokuwa matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 nchini Kenya hususan ya uchaguzi wa rais, inatarajiwa kuwa hayatakuwa chachu ya kuwazidishia Wakenya matatizo ya kiuchumi na kijamii, au mbaya zaidi, kuamsha mizimu ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilizoua watu zaidi ya 1,300 kwa mujibu wa takwimu rasmi za vyombo vya usalama nchini humo. Aidha machafuko hayo 2007 na 2008 yalipelekea maelfu ya watu kuachwa na majeraha ya daima, mbali na mamilioni ya wengine kufurushwa kwenye makazi, miji na vijiji vyao.”

  • Tags

You can share this post!

Mlima Kenya njia panda katika uchaguzi wa leo Agosti 9

Usalama kuimarishwa Kerio Valley

T L