Habari

Huu ndio wakati wa BBI – Uhuru

October 21st, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amesema ni lazima Wakenya wapitishe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na kurekebisha katiba kabla ya uchaguzi mkuu ujao ili kuondoa siasa za ushindani, la sivyo watajuta.

Rais alisema Ikiwa katiba haitafanyiwa marekebisho, huenda athari za ushindani zikaandama nchi kwa miaka mingi ijayo.

Akihutubu kwenye sherehe za Sikukuu ya Mashujaa mjini Kisii, Kaunti ya Kisii, Jumanne, Rais alisema ingawa Katiba ya 2010 ilitoa suluhisho kwa baadhi ya changamoto za kisiasa zilizokuwa zikiandama nchi, haikutatua tatizo hilo kikamilifu.

“Tusipobadilisha sasa wakati tuna fursa ya kugeuza katiba, tatizo hili litaendelea kusumbua nchi yetu kwa miaka mingi ijayo. Kwa hivyo, ninawaalika kwa mjadala wa kweli kuhusu hili. Na hatufai kuogopa kuchukua hatua za ujasiri jinsi waanzilishi wa taifa letu walifanya,” alisema Rais.

Rais Kenyatta alisema njia ya pekee kwa Kenya kufikia uthabiti wa kisiasa ni kupitia mageuzi ya kikatiba wala si chaguzi.

Alisema ukweli wa mambo ni kuwa, ghasia za kisiasa zilianza baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa 1992.

“Ujio wa mfumo wa vyama vingi mnamo 1992 ulituzalia tatizo la ushindani wa kisiasa usiofaa. Je, ni vipi tunatarajia kutatua suala hili kupitia chaguzi badala ya mageuzi ya kikatiba?

“Utakuwa mkasa mkuu ikiwa hatutakuwa tumesuluhisha tatizo hili kabla ya uchaguzi ujao. Ni kwa mantiki hiyo nawaomba wananchi kutathmini mchakato wa mageuzi ya kikatiba utakaokubalika na kumjumuisha kila mmoja,” akasema.

Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza umuhimu na haja ya kupitisha ripoti hiyo, akishikilia ndio njia pekee Kenya itaondoa ushindani wa kisiasa, ambapo anayeshinda hupata kila kitu huku yule anayeshindwa akiambulia patupu.

Kando na Rais Kenyatta, kinara wa ODM, Raila Odinga pia amekuwa akiipigia debe, kauli aliyoshikilia jana alipohutubu.

Hata hivyo, Naibu Rais William Ruto amekuwa akiipinga, akishikilia lengo lake kuu ni kubuni nafasi za uongozi kwa watu wachache.

Lakini jana, Rais Kenyatta alipinga dhana hiyo ya Dkt Ruto, akisema azma yake kuu ni kuhakikisha uwepo wa mfumo utakaomjumuisha kila mmoja.

“Hatupaswi kuendeleza fasiri zisizofaa kwamba, mpango wa mchakato huo ni kubuni nafasi kwa viongozi wachache. Ninachoomba ni mchakato wa kikatiba utakaojumuisha kila jamii baada ya uchaguzi. Mfumo ambao utampa nafasi anayeiongoza nchi kushirikiana na wenzake kutoka kila sehemu,” akasema Rais.

Alisema inasikitisha kuwa uchumi wa nchi huathirika kila baada ya uchaguzi, kwani lengo kuu la viongozi ni kupigania mamlaka ya kisiasa kwa kila hali.

“Mwaka mmoja kabla ya kila uchaguzi, hali ya uchumi ya nchi huathirika kutokana na mseto wa matarajio kuhusu matokeo yake. Hali huwa kama hiyo mwaka mmoja baada ya uchaguzi. Hilo linamaanisha kuwa, katika kila kipindi cha miaka mitano, huwa tunatumia miaka miwili kuangazia masuala yanayohusiana na matokeo ya uchaguzi,” akasema.

Mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta alikutana na viongozi wapya wa Bunge la Kitaifa na Seneti kujadili jinsi mabunge hayo yatashirikiana kupitisha miswada ya serikali ambayo imekwama.

Wadadisi wanasema hilo liliashiria kuandaa mazingira yafaayo kwa mabunge hayo kuipitisha ripoti hiyo bila pingamizi.

Licha ya hakikisho hilo, wadadisi wanaeleza macho yote ya Wakenya yatakuwa kwa mwelekeo wa kisiasa wa nchi, hasa baada ya Kenyatta na Odinga kukabidhiwa rasmi ripoti hiyo.

Jana, Dkt Ruto alisema mchakato huo unafaa kuhusisha kila Mkenya.