HabariSiasa

Huu si wakati wa kusaka kura za 2022 – Raila

August 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga Ijumaa aliwataka wanachama wa chama hicho wakomesha kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga aliwashauri kuelekeza juhudi zao katika kubuni njia za kukabiliana na changamoto zinazowasibu wananchi wakati huu.

“Huu sio wakati wa kuzunguka huku na kule mkisaka uungwaji mkono kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022. Huu ni wakati wa kushughulikia changamoto zinazowakabili raia kama vile kuzorota kwa uchumi, athari za mafuriko na ugonjwa hatari wa Covid-19,” akasema.

Bw Odinga alikuwa akiongea baada ya kufanya kikao cha faragha na viongozi kadhaa kutoka kaunti ya Siaya afisini mwake katika jumba la Capitol Hill, Nairobi.

Miongoni mwa wale waliokutana na Bw Odinga ni Seneta wa Siaya James Orengo, Mwanachama wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA) Oburu Oginga, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, Mkurugenzi Mkuu wa ODM Oduor Ong’wen miongoni mwa wengine.

Amri ya Bw Odinga inajiri baada ya ODM kuwafukuza baadhi ya viongozi wanaosawiriwa kuwa waasi wa chama hicho katika Kaunti ya Kisumu na ambao juzi walimtembelea Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi nyumbani kwake Eldoret.

Bw Sudi ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto. Alikutana na kundi hilo la vijana 200 kutoka eneo la Kondele kaunti ya Kisumu.

Wanachama waasi wa ODM waliofurushwa ni pamoja na Richard Ogembo ambaye zamani alihudumu kama waziri katika serikali ya kaunti ya Kisumu, Omollo Mberu, Jared Oriadha, Dan Nyamori, Peter Ogwel, Owino Mahawa na Maina Ochieng’.

Walikodi mabasi yalitowasafirisha zaidi ya vijana 200 kukutana na Bw Sudi pamoja na wanasiasa wengine wa mrengo wa Tangatanga.

Ujumbe huo umeratibiwa kukutana na Dkt Ruto nyumbani kwake Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu.

Bw Sudi alikutana na watu hao alipofanya ziara Kisumu mjini Kisumu ambapo wanasiasa hao walielezea nia ya kuvumisha azma ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022.

Bw Odinga ambaye amekuwa akiendelea kupona tangu aliporejea nchini kutoka Dubai ambako alifanyiwa upasuaji, pia alisema kuwa kuna uwezekano wa kura ya maamuzi kufanyika mwishoni mwa mwaka huu au mapema 2021.