Michezo

Huyu Mbappe atavunja rekodi zote za Messi na Ronaldo

November 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MAPEMA wiki jana, mshambuliaji nyota wa kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe alitajwa kuwa miongoni mwa wanadimba wenye uwezo wa kukua zaidi kwenye ulingo wa soka katika siku za usoni.

Shirikika CIES Observatory nchini Uingereza lilishikilia kwamba Mbappe ana kila sababu ya kuvuma pakubwa hata kuliko Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wanaopania kuzifikia sifa za kina Pele na Maradona.

Jarida la The Times nchini Amerika lilichapisha picha ya Mbappe kwenye ukurasa wake wa mbele na kuandika kuwa “tegemeo la siku za usoni katika ulingo wa soka duniani kote.”

Mbappe alianza kugonga vichwa vya habari mnamo Septemba 2017 baada ya kuridhisha sana kambini mwa AS Monaco na kuwa kivutio kikubwa cha PSG.

Miamba hao wa soka ya Ufaransa waliweka mezani kima cha Sh21 bilioni ili kumshawishi abanduke kambini mwa Monaco na kutua PSG akiwa bado ana umri wa miaka 18 pekee.

Kiini cha kuhemewa kwake hata na magwiji wa soka nchini Uhispania, Real Madrid ni ushawishi alioudhihirisha ndani ya jezi za Monaco ambao aliwachochea kutia kapuni ubingwa wa Ligue 1 na hivyo kukomesha ukiritimba wa PSG.

Mshahara wake tangu ahamie kambini mwa PSG umekuwa kima cha Sh48milioni kwa wiki na hivyo kuwa mchezaji wa pili baada ya Neymar Jr anayedumishwa kwa gharama ya juu zaidi katika kikosi kizima cha PSG.

Ushirikiano mkubwa na wafumaji wenzake katika safu ya mbele ya Ufaransa ulikuwa kiini cha Ufaransa kunyanyua ubingwa wa taji la Dunia chini ya kocha Didier Deschamps kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.

Mwishoni mwa michuano hiyo, Mbappe aliibuka Chipukizi Bora na ndiye aliyewafungia Ufaransa bao la pekee katika ushindi mwembamba wa 1-0 waliousajili dhidi ya Peru katika hatua ya makundi.

Kinda huyo kutoka mji wa Bondy viungani mwa jiji la Paris baadaye aliwapangua mabeki wa Argentina na kuwalaza miamba hao wa Amerika Kusini kwa mabao 4-3.

Kwa kufanya hivyo, Mbappe alikuwa mchezaji wa pili mwenye umri wa miaka 20 baada ya Pele mnamo 1958, kufunga mabao mawili katika mechi moja ya fainali za Kombe la Dunia.

Alipofunga bao katika fainali iliyowashuhudia wakiwapiga Croatia 4-2, aliweka rekodi ya kuwa kinda wa pili kufanya hivyo baada ya Pele mnamo 1958.

Mbappe alifunga jumla ya mabao manne kufikia mwisho wa fainali hizo na akatunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Kombe la Dunia la Fifa mnamo 2018.