Habari Mseto

Huzuni Kakamega wanafunzi 13 wakifariki shuleni

February 3rd, 2020 1 min read

Na BENSON AMANDALA

BIWI la simanzi Jumatatu lilitanda katika Kaunti ya Kakamega baada ya wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi ya Kakamega kuaga dunia shuleni huku  39 wakijeruhiwa.

Maafa hayo yalisababishwa na purukushani iliyozuka wanafunzi hao wakitoka madarasani kuelekea nyumbani.

Walikanyagana na wengine kuanguka kutoka orofa ya tatu.

Wanafunzi wengine 39 nao walipata majeraha mabaya na wanaendelea kulazwa katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kakamega huku wengine 20 wakitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Kamanda wa Polisi, ukanda wa Magharibi Peris Kimani alithibitisha idadi ya walioaga dunia katika kisa hicho cha kusikitisha nyakati za jioni.

Aidha, wazazi walikita kambi katika hospitali ya rufaa ya Kakamega wakiwatafuta wanao huku waliowapoteza watoto wao wakipiga nduru na baadhi hata kuzirai kwa kuzidiwa na machungu.

Hali ilikuwa mbaya zaidi hospitalini humo ikizingatiwa wahudumu wachache tu ndio walikwepo kutokana na mgomo unaoendelea wa madaktari katika gatuzi hilo.

Hadi tukienda mitambono, Kamishina wa kaunti ya Kakamega Pauline Dola na Bi Kimani walitarajiwa kuhutubia wanahabari kuhusu mauti hayo.