Habari za Kaunti

Huzuni miili ya mama kanisa ikifikishwa mochari ya Murang’a

February 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WINGU la simanzi lilitanda katika mochari ya Murang’a mnamo Jumanne wakati miili minne ya wanawake wahanga wa ajali ilipoletwa hapo.

Jamaa, marafiki, mapadri na mashahidi wengine walijitokeza katika mochari hiyo kupokea miili hiyo.

Baadhi ya akina mama wa Kanisa waliofika katika mochari ya Murang’a kupokea miili ya wenzao waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani mnamo Februari 4, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Akina mama hao wa Kanisa waliopoteza maisha walikuwa miongoni mwa 16 waliokuwa wakitoka kwa maombi spesheli katika Kaunti ya Nyandarua ambapo mwendo wa saa mbili usiku wakiwa katika barabara ya kutoka Nyahururu kuenda Nyeri, gari lao lilikumbana na ajali.

Walikuwa wa Kanisa Katoliki la Gaitega lililoko wadi ya Mbiri ndani ya eneobunge la Kiharu.

Baadhi ya jamaa, marafiki na waombolezaji wengine waliofika katika mochari ya Murang’a kupokea miili ya akina mama wa Kanisa waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani mnamo Februari 4, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Serikali ya Kaunti ya Murang’a ilisema iligharamia uchukuzi wa miili hiyo hadi Murang’a.

Ripoti za polisi kuhusu ajali hiyo zilionyesha kwamba kuna majeruhi sita ambao wamelazwa katika hospitali mbalimbali.

“Walio katika hospitali wana majeraha ya kuvunjika miguu, mikono, uti wa mgongo na yuko mwingine anayehitaji upasuaji wa tumbo,” ripoti hiyo yaonyesha.

[email protected]