Habari za Kaunti

Huzuni mwanafunzi akikwama migodini akisaka riziki

January 21st, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

HOFU imetanda katika kijiji cha Narworwo, Alale, Kaunti ya Pokot Magharibi baada ya mwili wa msichana mwenye umri wa miaka 15 kwenye migodi ya kuchimba dhahabu. 

Msichana huyo, Nakiru Ngolenyang inaarifiwa alikuwa miongoni mwa kundi la wanawake waliokuwa wakichimba dhahabu.

Akithibitisha tukio hilo kwa njia ya simu, Chifu wa Lokesheni ya Alale, Jackson Lokwakile alisema kuwa mnamo Jumatano (Januari 17, 2024), Nakiru alibainika kukwama migodini baada ya kukosekana kwenye orodha ya wanawake hao.

“Migodi ilipoporomoka, kina mama waliokuwa wakichimba dhahabu walitorokea usalama na kugundua baadaye msichana waliyekuwa pamoja hakuwepo,” Bw Lokwakile akasema.

Licha ya maafisa wa serikali kukabiliana na majanga pamoja na wale wa kaunti kuarifiwa kuhusu kukwama kwa msichana huyo, hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii hawakuwa wamewasili.

Familia na wakazi wamekita kambi katika eneo la mkasa kwa muda wa siku mbili mfululizo, bila mafanikio kufukua mwili wa mwathiriwa huyo.

“Migodi ilifumfumika na inatishia watu wengi ambao wamefika kuokoa,” alisema Chifu Lokwakile.

Akiongea na Taifa Leo Dijitali, Afisa wa mipango maalumu na majanga katika Kaunti ya Pokot Magharibi, David Chepelion alisema maafisa wa idara hiyo “wanashughulikua” suala hilo.

“Tuko katika harakati za kuelekea eneo la mkasa kufukua mwili wa mwathiriwa,” alisema.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kaunti/wachimbaji-madini-wapewa-mafunzo-kuepuka-vifo-migodini

Aliyekuwa mbunge wa Kacheliba, Mark Lomunokol alisikitika umaskini unashinikiza wakati kusaka riziki kwenye machimbo ya dhahabu.

“Hali ngumu ya maisha imeathiri kiwango kikubwa cha wakazi Pokot Magharibi. Isitoshe, mashambulizi yanayotekelezwa na wezi wa mifugo yamesababisha shule kufungwa hivyo basi wanafunzi kulazimika kushiriki uchimbaji dhahabu kwenye migodi,” alisema.

Alisema kuwa wazazi wanalazimika kupambana na hali ngumu ya maisha wakisaka mbinu mbadala kujikimu kwa sababu masoko ya mifugo yamefungwa.

“Hawana mahali pa kuuza mifugo ili wanunue chakula. Lazima wachimbe migodi ili wapate mlo. Shida kubwa ni kwamba wengi wao wanafunikwa kwenye machimbo na ni hatari sana hasa kwa watoto,” alisema.

Mbunge huyo wa zamani anaitaka serikali kuu kusambaza chakula kwa familia ambazo zimeathirika kutokana na baa la njaa.