Huzuni pacha wakifa baharini

Huzuni pacha wakifa baharini

Na SIAGO CECE

FAMILIA katika eneo la Gasi, Kaunti ya Kwale imegubikwa na simanzi baada ya watoto wao pacha kupatikana wamefariki baharini.

Miili ya wawili hao, Kennedy Gichui na Solomon Macharia wenye umri wa miaka 18, ilipatikana Jumanne asubuhi ambapo walikuwa wameshikana mikono.

Binamu yao, Kennedy Kamau, 16, ambaye alienda nao baharini Jumatatu jioni alifanikiwa kuogelea hadi akakwama kwenye mikoko, akaokolewa na wavuvi.

Alipookolewa ndipo akasema kuna wenzake wawili ambao alikuwa nao baharini. Alikimbizwa hadi Hospitali ya Kinondo kwa matibabu.

Akithibitisha kisa hicho, Mkuu wa Polisi wa Msambweni, Bw Fanuel Nasio alisema miili yao ilipelekwa kuhifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kwale.

Baba yao, Bw Samuel Njuguna ambaye ni mwashi mashuhuri Msambweni, alisema wavulana hao walikuwa wamekamilisha masomo ya Kidato cha Nne, mmoja akapata gredi ya C na mwingine C+.

“Walikuwa wanasubiri kujiunga na vyuo vikuu,” akasema Bw Njuguna.

Bi Clara Kanga, afisa wa uokoaji katika Kaunti ya Kwale ambaye aliongoza oparesheni ya uokoaji, alisema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na moja jioni siku ya Jumatatu.

Bi Kanga alisema wasingefanikiwa kuwatafuta Jumatatu jioni kwa sababu ya giza ndiposa wakalazimika kusubiri hadi Jumanne asubuhi.

Baada ya oparesheni iliyofanywa kwa saa mbili ikijumuisha wapigambizi, wavuvi na wenyeji, pacha hao walipatikana karibu na mikoko mwendo wa saa nne asubuhi.

“Walikuwa wameshikana mikono kumaanisha walikuwa wanajaribu kujiokoa. Mwili mmoja ulikuwa umeelea na mwingine ulikuwa bado umezama,” akaeleza.

Wanakijiji walisema watoto hao walienda kuogelea bila kujua kwamba maji huongezeka sana baharini hasa ifikapo jioni.

“Kuna sehemu ya bahari ambapo ni ghuba. Kwa vile wao ni wageni eneo hili, inawezekana waliendelea kuogelea bila kujua ghuba ingejaa maji,” akasema.

Msimamizi wa Kaunti Ndogo ya Msambweni, Bi Mwanakombo Kilalo, alisema kaunti ilikuwa imetoa ilani kwa wageni kuhakikisha wanaandamana na wenyeji ili wawe salama wanapoenda kuogelea au kutembea ufuoni.

“Nadhani waliona hapakuwa na maji baharini na hawakujua yangeongezeka ghafla,” akasema.

Kwingineko, polisi wanachunguza kisa ambapo mwanamume alifariki baada ya kumiminiwa risasi katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, karibu na mzunguko wa Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Bw Francis Kinuthia almaarufu Katoto, 50, ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri Mombasa alifariki papo hapo wakati alipomiminiwa risasi akiwa ndani ya gari lake usiku wa kuamkia Jumanne.

Mkuu wa polisi wa Changamwe, Bw David Mathiu, alisema gari ambalo halijatambuliwa lilikuwa likifuata gari la marehemu kabla amiminiwe zaidi ya risasi kumi.

Alisema kisa hicho kilitokea dakika chache baada ya saa mbili usiku wakati Kinuthia alipokuwa akielekea upande wa barabara ya Airport kutoka Changamwe.

Gari lake aina ya Toyota Premio lilipelekwa hadi kituo cha polisi cha Changamwe. Lilimiminiwa risasi upande wa kulia.

Bw Mathiu alisema polisi wameanzisha uchunguzi ili kuwatafuta waliohusika na kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Mwezi uliopita, kisa kama hicho kilitokea karibu na sehemu hiyo hiyo ambapo watu watatu walifariki baada ya gari lao kumiminiwa risasi zaidi ya 20.

You can share this post!

Rais ashauri mahakama itumie hekima

Saint George Ethiopia, Wakenya watakia Matasi afueni baada...