Habari

Huzuni watu 10 wakifa maji ziwani

November 18th, 2020 1 min read

Na DICKENS WASONGA

BIWI la simanzi lilitanda katika ufuo wa Ziwa Victoria, eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya baada ya watu 10 kufa maji usiku wa kuamkia Jumatano.

Kufikia Jumatano, maafisa kutoka idara ya ulinzi wa pwani za Kenya walikuwa wanaendelea kutafuta miili ya waliozama.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Siaya, Bw Francis Kooli alithibitisha kisa hicho.

Bw Kooli alisema kwamba merikebu hiyo ilikuwa na abiria 20 wakati ilipozama saa tano usiku Jumanne.

Chombo hicho kiligongwa na mawimbi makali yaliyoandamana na dhoruba na kuzama karibu na eneo la Muda katika ufuo wa Honge, mjini Bondo.

Kisa hicho kiliripotiwa kwa polisi katika Ufuo wa Usenge na Bw Zachary Masinde ambaye ni mwenyekiti wa ufuo wa Honge.

“Kulingana na mwenyekiti huyo wa ufuo, merikebu ya Uganda ilikuwa inatoka kwenye ufuo unaofahamika kama Ufuo wa Nairobi katika taifa hilo jirani, ikiwa imebeba abiria 20,” alisema Bw Kooli.

Abiria hao walikuwa wafanyabiashara waliokuwa wamebeba ndizi na matunda wakielekea katika ufuo wa Usenge.

“Mawimbi makali yaligonga boti hiyo ilipokuwa ikikaribia ufuo wa Honge. Ilizama mara moja,” alisema.

Bw Masinde alieleza Taifa Leo kwamba watu 10 waliokolewa na wavuvi waliokuwa ziwani humo kwenye shughuli za uvuvi.

“Kwa bahati nzuri kulikuwa na wavuvi waliokuwa karibu na wakamudu kuwaokoa baadhi ya abiria,” alisema.

Polisi waliwatambulisha walionusurika mkasa huo kama Bw Sadam Idrissa, 44, Bw Mathius Stephen, 62, Bw Henry Shitindi, 33, Bw Kudamba Issa, 42, na Bw Wafula James 39.

Wengine ni pamoja na Bi Annette Kawara, 42, Bi Morine Amukula, 22, Bw Alex Opiyo, 36, Bw Kevin Kalai, 42, na Hailat Kauma, 30, wote ambao ni raia wa Uganda.

Waliozama walijumuisha nahodha wa merikebu hiyo.