Michezo

IAAF yaitambua rasmi rekodi ya dunia ya Kipruto katika mbio za masafa ya kilomita 10

May 15th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

AKIWA na umri wa miaka 20 pekee, mwanariadha Rhonex Kipruto ameanza kutia maguu yake katika jukwaa la wafalme wa mbio za masafa marefu duniani.

Hii ni baada ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kurasimisha rekodi yake ya muda wa dakika 26:24 kwenye mbio za kilomita 10; ufanisi alioufikia aliposhiriki kivumbi cha Valencia Ibercaja nchini Uhispania mwaka 2019.

Bingwa huyo wa dunia katika mbio za mita 10,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, kwa sasa analenga kutia kapuni nishani ya dhahabu katika michezo ijayo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan.

Rhonex, 20, alivunja rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 10 mwezi mmoja tu baada ya Mganda Joshua Cheptegei kukamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 26:38 jijini Valencia mnamo Disemba 2019.

Kipruto alitawala mbio hizo tangu mwanzo na alifikia hatua ya kilomita tatu baada ya muda wa dakika 7:59 pekee, kabla ya kusalia peke yake uongozini.

Alifikia katikati ya kivumbi hicho baada ya muda wa dakika 13:18, akijivunia sekunde nne chini ya rekodi ya muda wa dakika 13:22 uliotumiwa na Mkenya Robert Keter kufikia hatua hiyo katika kivumbi kilichoandaliwa Lille, Ufaransa mnamo Novemba 9, 2019.

Kwa kusajili muda wa dakika 26:24, Kipruto ambaye ananolewa na kocha Colm O’Connell, alinyofoa sekunde 14 zaidi kwenye rekodi ya dakika 26:38 iliyokuwa ikishikiliwa na Cheptegei.

Kipruto ambaye kwa sasa anajishughulisha na upanzi a miche katika kijiji cha Kimamet, eneo la Kamwosor, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet, anapigiwa upatu wa kushindia Kenya nishani ya dhahabu katika Olimpiki za Tokyo, Japan mwakani.

Kenya ilijishindia medali hiyo mara ya mwisho katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki za 1968 kupitia kwa Naftali Temu nchini Mexico.

Kipruto ni kakaye mkubwa mwanariadha Bravin Kogei anayeinukia vyema katika mbio za kilomita 10 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20.

Tangu Machi 13, 2020 ambapo kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipothibitishwa humu nchini, shughuli zote za michezo zilisitishwa na serikali – hatua ambayo Kipruto anasema ilimweka katika ulazima wa kujishughulisha na masuala mengineyo yakiwemo kilimo na ufugaji baada ya kambi yao ya mazoezi kufungwa.