Michezo

Ibra apatikana na virusi vya corona

September 24th, 2020 1 min read

NA MASHIRIKA

MILAN, Italia:

Mshambuliaji wa AC Milan Zlatan Ibrahimovic amepatikana na virusi vya corona, klabu hiyo ya Ligi Kuu Italia (Serie A) imethibitisha Alhamisi.

Tangazo hilo limetolewa saa chache kabla ya miamba hao wa Italia kuvaana na klabu ya FK Bodo/Glimt kutoka Norway katika mechi ya raundi ya tatu ya kufuzu kushiriki Ligi ya Uropa mnamo Alhamisi.

Milan inasema kuwa imefahamisha “vyombo vinavyostahili kufahamishwa” na kuwa raia huyo Mswidi sasa ataanza karantini ya lazima nyumbani kwake.

Klabu hiyo iliongeza kuwa hakuna mchezaji mwingine ama afisa katika klabu hiyo amepatikana na virusi hivyo katika awamu ya upimaji wa virusi hivyo ya hivi punde, ingawa beki Leo Duarte alipatikana na virusi hivyo Jumatano na tayari amejitenga.

Ibrahimovic, ambaye anamiliki asilimia 23.5 ya klabu ya Hammarby nchini Uswidi, amefungia Milan mabao matatu katika mechi mbili za kwanza za msimu huu wa 2020-2021.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38, ambaye ana utajiri wa Sh21.1 bilioni, alijiunga na Milan kwa kandarasi ya mwaka mmoja baada ya kufanya vyema aliporejea katika klabu yake mwezi Januari 2020 akitokea LA Galaxy.

TAFSIRI NA GEOFFREY ANENE