Ibrahimovic afikisha mabao 500 na kuongoza AC Milan kurejea kileleni mwa jedwali la Serie A

Ibrahimovic afikisha mabao 500 na kuongoza AC Milan kurejea kileleni mwa jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Zlatan Ibrahimovic, 39, alipita idadi ya mabao 500 ambayo ameyafunga kwenye soka ya ngazi ya klabu baada ya kupachika wavuni magoli mawili mnamo Jumapili usiku na kusaidia waajiri wake AC Milan kucharaza Crotone 4-0 kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Ushindi huo wa AC Milan uliwarejesha kileleni mwa jedwali kwa alama 49, mbili zaidi kuliko nambari mbili Inter Milan.

Bao lililofungwa na Ibrahimovi kunako dakika ya 30 lilikuwa lake la 500 akivalia jezi za klabu mbalimbali katika ulingo wa soka.

Nyota huyo ambaye amewahi pia kuchezea Malmo FC, Ajax, Juventus na Inter Milan, alipachika wavuni goli lake la 501 na la 11 kutokana na mechi 11 za Serie A msimu huu katika dakika ya 64 kabla ya Ante Rebic kufungia AC Milan mabao mengine mawili kunako dakika za 69 na 70 mtawalia.

Ibrahimovic amewahi pia kuchezea Barcelona, Paris Saint Germain (PSG), Manchester United na LA Galaxy ya Amerika.

Huku AC Milan wakidhibiti sasa kilele cha jedwali la Serie A kwa pointi 49, saba mbele ya mabingwa watetezi Juventus, Crotone wanakokota nanga mkiani kwa alama 12 kutokana na mechi 21 zilizopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mbwa apima corona kwa ufanisi mkuu

Teddy Akumu na timu yake ya Kaizer Chiefs yaduwazwa na...