Michezo

Ibrahimovic afunga bao kuisaidia AC Milan kuwapepeta Lazio 3-0

July 5th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI mkongwe Zlatan Ibrahimovic alifunga bao na kusaidia AC Milan kuwapepeta Lazio 3-0 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Matokeo hayo yaliwayumbisha Lazio kabisa na kuwaweka Juventus pazuri zaidi kutia kibindoni ufalme wa taji la Serie A kwa msimu wa tisa mfululizo.

Ibrahimovic, 38, aliwafungia Milan bao la pili kupitia penalti katika dakika ya 34 baada ya Hakan Calhanoglu kuwaweka kifua mbele kunako dakika ya 23. Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Ibrahimovic kusakata tangu apate jeraha baya la mguu litakalomweka mkekani tangu mwishoni mwa Mei, 2020.

Fowadi Ante Rebic alikizamisha kabisa chombo cha Lazio kwa kufungia Milan goli la tatu katika dakika ya 59. Zikisalia mechi nane zaidi kwa kipute cha Serie A kutamatika rasmi msimu huu, Lazio wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 68, saba nyuma ya viongozi Juventus wanaonolewa na kocha Maurizio Sarri.

Milan kwa upande wao wanashikilia nafasi ya sita huku wakiwa na matumaini ya kufuzu kwa kipute cha Europa League msimu ujao. Hata hivyo, wana kibarua kizito cha kuepuka presha ya Napoli wanaowasoma mgongo kwa karibu sana.

MATOKEO YA SERIE A (Julai 4, 2020):

Juventus 4-1 Torino

Lazio 0-3 AC Milan

Sassuolo 4-2 Lecce